Ruka hadi kwenye maudhui makuu

YANGA YAZIDI KUJIKITA KILELENI, SIMBA NAFASI YAKE NI YA TATU

Mabingwa wa bara Yanga wamejiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia ushindi mnono wa magoli 3-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya, huku mahasimu wao, Simba, wakihitimisha ziara ya mkoani Tanga kwa kuzoa pointi zote sita baada ya kuifunga Mgambo 2-0 jana.

Washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam, nao walishinda mechi yao ya pili mfululizo jana baada ya kuibwaga Stand United kwa magoli 2-0 na kujiimarisha katika nafasi pili.

Kulikuwa na ushindi mwingine mkubwa mjini Mbeya wakati wenyeji Mbeya Ciy walipowasambaratisha JKT Ruvu kwa magoli 3-0 kwenye Uwanja wa Sokoine.

Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, beki wa kati wa kimataifa wa Yanga kutoka Rwanda, Mbuyu Twite, ndiye aliwafungia mabingwa hao watetezi bao la kwanza katika dakika ya 27 akiwahi mpira uliotemwa na kipa wa Prisons, Mohammed Yusuph. Kipa huyo alitema mpira wa ‘fri-kiki’ uliopigwa na Haruna Niyonzima.

Sekunde chache kabla ya kwenda mapumziko, Mrundi, Amissi Tambwe, aliipatia Yanga bao la pili kwa kichwa akiwahi mpira wa faulo uliopanguliwa na kipa wa Prisons, Mohammed Yussuf.


Mzimbabwe Donald Ngoma aliifungia Yanga bao la tatu kwa njia ya penalti katika dakika ya 60 baada ya Refa, Alex Mahaggi, kutoka Mwanza kutoa adhabu hiyo kufuatia Msuva kuangushwa ndani ya boksi akiwa anaelekea kufunga.

Kabla ya kutoa penalti hiyo, Mahaggi, alimuonyesha kadi nyekundu beki wa Prisons, James Josephat, ambaye awali alikuwa na kadi ya njano. Simba ililifunika kabisa jinamizi la kukosa matokeo kwenye uwanja wa Mkwakwani baada ya jana kupata ushindi wa pili mfululizo kupitia magoli ya kiungo Mzimbabwe Justice Majabvi na ‘straika’ Mganda Hamis Kiiza.

Simba walipata goli lao la kwanza katika dakika ya 27 kupitia kwa kiungo wake, Majabvi aliyeunganisha mpira wa kona uliopigwa na Peter Mwalyanzi kabla ya Kiiza aliyeingia kuchukua nafasi ya Awadhi Juma kutupia goli la pili kufuatia piga nikupige langoni mwa Mgambo na kuilipia kisasi timu yake ambayo msimu uliopita ililala 2-0 dhidi ya Mgambo uwanjani hapo.

Mafanikio hayo yalifuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya African Sports Jumamosi iliyopita, ambao ulikuwa wa kwanza na goli lao la kwanza Mkwakwani kwa miaka minne iliyopita. Kabla ya ushindi wa Jumamosi, Simba ilikuwa haifunga goli lolote uwanjani hapo tangu Agosti 24, 2011 waliposhinda 1-0 dhidi ya Coastal Union kupitia bao la Patrick Mafisango, ambaye sasa ni marehemu.

Kwenye Uwanja wa Kambarage, mabingwa wa mwaka juzi, Azam waliibwaga Stand United 2-0 kupitia goli la straika mpya Mkenya, Allan Wanga, na la kiungo Frank Domayo, ukiwa ni ushindi wao wa pili mfululizo msimu huu baada ya kuifunga Prisons ya Mbeya 2-1 katika ufunguzi wa msimu kwenye Uwanja wa Azam Complex Jumamosi iliyopita.

Kikosi cha Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Haji, Nadir Haroub ‘ Cannavaro’, Kelvin Yondani, Thabani  Kamusoko, Saimon Msuva, Haruna Niyonzima/ Geofrey Mwashiuya (dk.81), Amissi Tambwe/ Malimi Busungu (dk.85), Donald Ngoma na Deus Kaseke/ Salum Telela (dk 66).

Simba: Manyika Peter, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Kessy, Juuko Mursheed, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Awadhi Juma/Hamis Kiiza (58), Said Ndemla/Papa N’daw (86), Mussa Mgosi/ Ibrahim Hajibu, Mwinyi Kazimoto, Peter Mwalyanzi.

Matokeo kamili ya mechi za jana za Ligi Kuu ya Tanzania Bara:

Yanga 3-0 Prisons
Mgambo 0-2 Simba
Stand United 0-2 Azam
Mbeya City 3-0 JKT Ruvu
Ndanda 1-0 Coastal Union
Toto 1-2 Mtibwa
Mwadui 2-0 African Sports
Majimaji 1-0 Kagera Sugar

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC