Ruka hadi kwenye maudhui makuu

SIMBA NA YANGA TIKETI ZA KIELEKTRONIKI LAZIMA- TFF

Serikali imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuendelea kutumia tiketi za elektroniki licha ya klabu kongwe nchini Simba na Yanga kukataa kutumia tiketi hizo katika mechi yake ya kwanza ya watani wa jadi msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Mwishoni mwa mwezi uliopita viongozi wa Simba na Yanga walikubaliana kwa pamoja kukataa tiketi za elektroniki kutumika katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba 18, mwaka huu wakidai mfumo huo una changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kuwafanya wachelewe kupata mapato yao.


Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuwa, tiketi za elektroniki zitaendelea kutumika katika mechi za soka nchini ili kutekeleza agizo la serikali lililotolewa miezi minne iliyopita.

"Jana (juzi) hapa wizarani tulikutana na uongozi wa TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kuzungumzia msuguano unaoendelea kwa sasa kuhusu uamuzi wa TFF kutaka kukata asilimia tano ya fedha za udhamini wa klabu. Tumewaambia waache malumbano kwenye vyombo vya habari, wakae chini na kutatua tatizo kwa njia sahihi ya mazungumzo," Nkamia alisema.

"Tulizungumzia pia kitendo cha viongozi wa Simba na Yanga kugomea tiketi za elektroniki katika mechi baina ya timu zao itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa. Kukataa tiketi za elektroniki si sawa maana zipo kisheria na matumizi yake ni agizo la serikali, wajadili namna ya kutatua changamoto zilizojitokeza na si kukataa matumizi yake.


"Lengo la kuwaita wizarani lilikuwa ni kuwaeleza msimamo wa serikali kuhusu mgogoro uliopo katika soka la Tanzania. Wamekubaliana pande zote mbili kwa maana ya TFF na Bodi ya Ligi Kuu kukutana Dar es Salaam Jumamosi ya wiki hii kuzungumzia masuala hayo."

Nkamia ambaye pia ni Mbunge wa Chemba (CCM), aliwataja baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao cha juzi kilichofanyika kwenye ofisi za wizara hiyo zilizopo Posta jijini Dar es Salaam kuwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, Wilfred Kidau, wote wakiwakilisha TFF na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Silas Mwakibinga aliyewakilisha bodi hiyo.

AGIZO LA BUNGE
Utumiaji wa tiketi za kielektroniki ni utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya Kamati Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha Mapato ya TFF iliyotolewa 2011 na agizo la serikali lililotolewa katikati ya mwaka huu.

Mei 2011 kamati hiyo iliyoongozwa na Rais Mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga, ilitoa ripoti yenye kurasa 95 ikionesha uhujumu mkubwa wa mapato ya milangoni utokanao na matumizi ya tiketi za kawaida, hivyo kamati ikapendekeza TFF ianze kutumia tiketi za kisasa za kielektroniki.

Aidha, Juni mwaka huu, serikali iliiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuiamuru TFF kutumia mfumo wa tiketi za kielektroniki kwenye viwanja mbalimbali vya soka nchini ili kudhibiti uhujumu wa mapato ya milangoni.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa fedha 2014/15 bungeni mjini Dodoma Juni 4, mwaka huu, mwenyekiti wa kamati hiyo, Luhaga Mpina aliitaka TRA kutoa sharti kwa TFF kutumia mfumo wa tiketi za elektroniki ili kuongeza mapato ya nchi.

"Ni kwa muda mrefu serikali imekuwa haipati mapato ya kutosha kutoka katika sekta ya michezo hususan mpira wa miguu ulio chini ya TFF. Hii inatokana na mfumo dhaifu wa ukusanyaji fedha kipindi cha uuzaji tiketi, mfano tiketi bandia kuendelea kutumika, kukosekana kwa uwazi katika mapato halisi, uwezo mdogo wa kusambaza tiketi nchi nzima na rushwa kwenye mageti," alisema Mpina.

"TFF iliona changamoto hiyo na kuamua kutangaza zabuni ya tiketi za elektroniki mwaka 2012 ambayo Benki ya CRDB ilishinda na tayari imekwishatayarisha na kuweka mfumo huo kwa gharama ya Sh. bilioni tatu tangu mwaka 2013.

"Kamati inashauri TRA iweke sharti la lazima la kuitaka TFF kutumia mfumo wa tiketi za kielektroniki katika kuuza tiketi zake ikiwa ni jitihada za kuongeza mapato ya serikali," alisema Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa (CCM).

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC