Ruka hadi kwenye maudhui makuu

TAIFA STARS WAPAA, TAYARI KULIPIZA KISASI KWA BURUNDI

Kikosi chenye wachezaji 20 cha timu ya taifa (Taifa Stars) kimeondoka nchini leo alfajiri kwenda Bujumbura, Burundi huku kocha wa timu hiyo, Mholanzi Mart Nooij akiahidi kulipa kisasi cha kufungwa 3-0 dhidi ya taifa hilo katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya 'Entamba Murugamba' itakayopigwa nchini humo Jumapili.

Katika mechi iliyopita ya kirafiki iliyozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Aprili 26, mwaka huu, kikosi cha Taifa Stars kilichokuwa "kimefinyangwafinyangwa" na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kulazimisha waanze wachezaji watano wa 'maboresho', kililala 3-0 dhidi ya Warundi na kuharibu pilau la sherehe zilizokuwa zimefana za Miaka 50 ya Muungano.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa kuagwa kwa Taifa Stars, Nooij alisema amekiandaa vyema kikosi chake kuhakikisha kinaibuka na ushindi ili kulipa kisasi cha kufungwa nyumbani na pia kujihakikishia kinapanda katika viwango vya soka vya kimataifa vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

"Ninatambua Burundi ina wachezaji wazuri na wa kimataifa kina (Amisi) Tambwe, (Pierre) Kwizera na (Didier) Kavumbagu lakini kwa kikosi tunachokwenda nacho, tuna uhakika wa kushinda ugenini na kulipa kisasi maana walitufunga kwetu," alisema Nooij.

Aliwataja wachezaji 20 anaokwenda nao Bunjumbura kuwa ni pamoja na makipa Mwadin Ally (Azam FC) na Deogratias Munishi 'Dida' (Yanga).

Wengine ni Shomari Kapombe (Azam FC), Oscar Joshua (Yanga), Said Morad (Azam FC), Nadir Haroub 'Canavaro' (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Joram Mgeveke (aliyesajiliwa Simba kutoka kikosi cha maboresho ya Taifa Stars), Simon Msuva (Yanga), Erasto Nyoni (Azam FC), Himid Mao (Azam FC), Amri Kiemba (Simba), Haruna Chanongo (Simba), Salum Abubakary 'Sure Boy' (Azam FC), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya ya Qatar), Hamis Mcha (Azam FC), Juma Luizio (Zesco FC ya Zambia), Mrisho Ngasa (Yanga), Mbwana Samata na Thomas  Ulimwengu (wote TP Mazembe ya DRC).

Nooij alisema mshambuliaji na nahodha wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor', beki kisiki Agrrey Morris na kipa Aishi Manula wameachwa katika msafara wa Burundi kwa sababu mbalimbali zikiwamo majeraha na kutokuwa na uhakika wa kucheza Jumapili.

Alisema Bocco na Morris ni majeruhi huku akieleza kuwa makipa Dida na Mwadini wanatosha kwa mechi hiyo, hivyo haoni sababu ya kwenda na Manula.
Stars itaingia uwanjani mwishoni mwa wiki ikiwa na kumbukumbu ya kutolewa na Zimbabwe kwenye mbio za kuwania kushiriki fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Morocco mwakani.

Naye Somoe Ng'itu anaripoti kuwa washambuliaji wawili wa kimataifa wa Simba, Amissi Tambwe, Pierre Kwizera na Didier Kavumbagu wa Azam, waliondoka nchini jana na kuelekea kwao Burundi kwa ajili ya kujiunga na timu yao ya taifa inayojiandaa kuivaa Taifa Stars keshokutwa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema kuwa Tambwe, Kwizera na nyota wengine wa Taifa Stars walipewa ruhusa jana kwa ajili ya kujiunga na timu zao za taifa.

Matola alisema kuwa hata hivyo, kuondoka kwa nyota hao hakutaharibu programu ya mazoezi kwa sababu huko wanapokwenda pia wanakwenda kucheza mechi ya kimataifa.

"Kwa upande wetu tuko vizuri, kikosi kimeiva na msimu ujao tutatoa ushindani kwa kila tutakayekutana naye," alisema Matola.
Taifa Stars na Burundi zinakutana katika mchezo unaotambuliwa na kalenda ya FIFA.

Tayari wachezaji wanaocheza nje ya nchi, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Mwinyi Kazimoto anayecheza klabu ya Al Markhiya ya Qatar wameshawasili nchini.

Awali Stars ilitarajia kucheza dhidi ya Morocco lakini Waarabu hao waliikacha wakidai kwamba wamewakosa nyota wao wanaocheza nje ya nchi hiyo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC