Ruka hadi kwenye maudhui makuu

ROBO FAINALI KOMBE LA KAGAME NI KUSUKA AU KUNYOA

KAMA refa Israel Mujuni angekuwa sahihi, bila shaka Gor Mahia ingekuwa moja ya timu zilizofuzu Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka huu mjini Kigali, Rwanda.

Lakini kwa makosa ya kibinadamu, akakataa bao safi la tatu la Gor katika mchezo wa Kundi B dhidi ya APR na mwisho wa mchezo, timu hizo zikatoka sare ya 2-2.

Gor ilihitaji kushinda mechi mbili za mwisho za kundi lake dhidi ya APR na Telecom ya Djibouti, baada ya kufungwa mechi mbili za awali na KCC ya Uganda na Atletico ya Burundi ili iende Nane Bora, lakini ikaambulia pointi mbili katika mechi hizo kwa sare ya 2-2 kila mchezo.

Gor iliingia katika mchezo dhidi ta Telecom ikiwa tayari inajua KQ inawasubiri Uwanja wa Ndege wa Kigali kuwarejesha Nairobi- hivyo walikuwa hawana cha kupigania.


Kwa maana ya mashindano, Gor walimaliza katika mechi na APR na walirudi Uwanja wa Nyamirambo jana kukamilisha ratiba. Lakini wengi hawajafurahishwa kutolewa kwa timu hiyo inayofundishwa na Mscotland, Bobby Williamson.

Kwa sababu ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri na katika mechi zake zote ilikosa bahati tu, ilikuwa inatengeneza nafasi nyingi, inashindwa kutumia na katika mchezo dhidi ya APR refa wa Tanzania Bara aliwamaliza kwa kukataa bao lao.

Gor Mahia ilikaribia kabisa kupata ushindi wa kwanza katika michuano ya mwaka baada ya kutoka nyuma kwa bao 1-0 kipindi cha kwanza na kuongoza kwa 2-1 hadi sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho.

Hata hivyo, bao la dakika ya 90 na ushei la Bernabe Mubumbi akimalizia krosi ya Jean Baptiste lilizima ndoto hizo na kulazimishwa sare ya 2-2. Siku hiyo, Jean Claude Mugiraneza alitangulia kuifungia APR dakika ya 22 kabla ya Godfrey Kizito kusawazisha dakika ya 60 na Godfrey Walusimbi kufunga la pili dakika ya 84.

Dan Sserunkuma aliifungia bao la tatu Gor dakika ya 88, baada ya kipa wa APR kuutema mpira mrefu wa kichwa wa kurudishiwa na mshambuliaji huyo akauchukua na kuutupia nyavuni, lakini refa Israel Mujuni akakataa, kwa dhana mlinda mlango alipamiwa.

Bobby Williamson aliondoka Uwanja wa Nyamirambo kwa hasira akiwabwatukia marefa. “Soka ni soka, lakini huyu refa na mshika kibendera wake wamefanya tufungwe hawafai kabisa hawa watu, mchezaji kaangushwa pale, hakupiga filimbi, mpira umeendelea kuchezwa hadi tumefungwa (bao la kusawazisha) ”alisema kwa hasira Bobby na kuondoka zake.
Jambo moja tu unaloweza kusema juu ya kuondolewa kwa Gor, ni walikosa bahati.

TAJI LIKO WAZI, MABINGWA WAREJEA NYUMBANI MAPEMA

Vital’O walirithi taji lililoachwa wazi na Yanga SC mwaka jana ambao waligoma kwenda Sudan wakihofia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyokuwa yakiendelea huko.

Baada ya ushindi huo, mfungaji wao tegemeo, Amisi Tambwe akanunuliwa na Simba SC ya Tanzania Bara, ambako amekwenda kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya nchi hiyo pia.

Hakuna kilichowezekana kwa Vital’O bila Tambwe Mabao, imetolewa mapema katika hatua ya makundi na kuacha taji lishindaniwe na timu nane, Azam, APR, Atlabara, Atletico, El Merreikh, Polisi, KCC na Rayon.

Timu nyingine zilizoishia hatua ya makundi ni KMKM ya Zanzibar, Adama City ya Ethiopia, Benadir ya Somalia na Telecom ya Djibouti.

ROBO FAINALI NI ZA KUKATA NA SHOKA.

Kwa wanaoijua vyema soka ya Afrika Mashariki na Kati, hapana shaka wanajua ubora wa El Merreikh ya Sudan- sasa itakutana na Azam FC ya Tanzania Bara katika Robo Fainali.

Azam ni timu nzuri, inacheza vizuri na ni miongoni mwa timu zinazotabiriwa kutwaa Kombe mwaka huu, lakini ukweli ni kwamba, kukutanishwa na Merreikh ni sawa na kupitishwa daraja bovu, ambalo halikawii kuwadondosha.

Azam FC wakivuka mtihani huo- wazi watakuwa wamefuzu zoezi gumu kuelekea kutwaa taji la kwanza la michuano ya mabingwa wa CECAFA.

Merreikh pia inaweza kupata mbeleko ya marefa dhidi ya Azam kutokana na umoja na upendo uliopo baina nchi wanachama wa CECAFA zinazozungumza Kiarabu, ambazo ni Sudan, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini, Eritrea na Djibouti.

Na katika michuano hii asilimia kubwa ya marefa wanatoka nchi hizo- na tayari imeonekana katika mechi za makundi umoja huo ukifanya kazi vizuri.

Israel Mujuni amejenga mazingira ya Wakenya kuichukia Tanzania baada ya kukataa bao zuri la Gor Mahia dhidi APR, marefa wa Rwanda hakuna uhakika kama watapenda Azam iende Nusu Fainali, labda Waganda.

Wazi Azam itapitia katika mtihani mgumu- jambo ambalo wanapaswa kulitambua mapema ili ‘wakaze msuli’ haswa kama wanataka kurejea na Kombe Dar es Salaam.

APR na Rayon ni wapinzani wa jadi katika soka ya Rwanda- na kesho itapigwa mechi yenye msimsiko zaidi ya zote kwenye mashindano haya Uwanja wa Nyamirambo.

Polisi na askari wa jeshi la Rwanda pia watasimama katikati ya mashabiki wa APR na Rayon kuhakikisha hawagusani- Uwanja utafurika mno na wachezaji wataonyeshana kazi.

Wenyeji wa hapa wanasema ni mechi ambayo imekuja mapema, angalau ingekuja katika hatua ya Nusu Fainali- lakini kwa kuwa ndiyo imeshakuwa hakuna namna- acha kinukishwe kesho Nyamirambo.

Wachezaji wa Gor Mahia na Telecom katika mchezo wa jana Nyamirambo uliomalizika kwa sare ya 2-2
Wachezaji wa KCC na APR katika mchezo wa jana ambao timu ya Uganda ilishinda 1-0

Rahisi sana kutabiri matokeo ya Robo Fainali nyingine kwamba Polisi itaitoa Atletico na KCC itaitoa Atlabara, lakini katika soka lolote linawezekana na matokeo yakawa tofauti.

Hadi sasa, timu yoyote itakayoingia Nusu Fainali inaweza kutwaa na Kombe pia- kwa kuwa viwango havipishani sana. Moto utawaka kesho baina ya wana Mji wa Kigali- APR na Rayon, ila Azam wamepitishwa daraja bovu kwa Merreikh, wavuke kwa tahadhari.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC