Ruka hadi kwenye maudhui makuu

WAMBURA AZIDI KUKINUKISHA MSIMBAZI, SASA KUMBURUZA NDUMBARO TFF

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa shirikisho la soka nchini, Michael Wambura, ambaye anapinga kuenguliwa katika uchaguzi mkuu wa Klabu ya Simba, amesema atamburuza Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Damas Ndumbaro, kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kufuatia 'kumpakazia' kashfa ya kughushi nyaraka na pia kumtukana.

Wambura alisema katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari jana kuwa anawasilisha malalamiko yake katika Kamati ya Maadili ya TFF ili ukweli wa mambo ufahamike.

"Kwa kuwa nimeshakata rufaa TFF kupinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba, busara inanielekeza kutolumbana na na kujibizana na Ndumbaro ili kuipisha Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF ifanye maamuzi yake," alisema katika taarifa yake hiyo.

Aliongeza: "Kwa mambo ambayo hayana uhusiano na uchaguzi kama kughushi nyakara, matusi na kashfa mbalimbali mambo hayo nitayawasilisha kwa Kamati ya Madili ya TFF ili ukweli ufahamike na hatua zichukuliwe na baada ya hapo vyombo vya dola vinavyohusiana na kutambua maandishi vipewe nafasi ya kufanya kazi yake."


Kisha akawataka wanachama wa Simba kuwa na subira wakati vyombo husika vikifanya kazi yake na akasisitiza; "ni imani yangu ukweli utakuwa wazi na haki itapatikana."

Simba inatarajia kufanya uchaguzi wake Juni 29 mwaka huu kufuatia viongozi walioko chini ya Mwenyekiti, Ismail Aden Rage, kumaliza muda wao.

Wagombea wengine waliopitishwa baada ya usaili ni Geofrey Nyange 'Kaburu', Swedy Mkwabi, Jamhuri Kihwelo 'Julio' na Bundala Kaburwa wanaowania nafasi ya Makamu wa Rais.

Nafasi ya Ujumbe ni Ally Suru, Abdulhamid Mshangama, Alfred Elia, Chano Almasi, Amina Poyo, Asha Muhaji, Collins Frisch, Ally Chaurembo, Daniel Manembe, Khamis Mkoma, Ibrahim Masoud 'Maestro', Iddi Mkambala, Addi Kajuna, Jasmin Badar, Juma Mussa, Maulid Abdallah, Rodney Chiduo, Said Kubenea, Ibrahim Masoud ‘Maestro’, Said Pamba, Said Tully na Yasin Mwete.

Wakati huo huo, TFF imesema kwamba bado haijawataarifu wajumbe wa Kamati ya Rufaa kwa ajili ya kukutana kujadili rufaa iliyowasilishwa na Wambura, ambaye anapinga kuenguliwa katika uchaguzi mkuu wa Klabu ya Simba.

Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, alisema kwamba bado sekretarieti ya shirikisho hilo haijaamua ni kamati ipi inastahili kujadili rufaa ya Wambura ambayo ndani ameeleza hoja zake 14 za kupinga kuondolewa.

Mwesigwa alisema kwamba kwa sasa TFF inaendelea kuweka sawa taratibu zinazohusiana na kikao hicho cha kujadili rufaa hiyo na wataitisha kikao kwa kuzingatia kalenda ya uchaguzi ya klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi.

“Bado hatujajua lini itajadiliwa na hatujaamua itajadiliwa na kamati ipi, ila imeshaanza kufanyiwa kazi katika ngazi ya sekretarieti, ” alisema kwa kifupi Mwesigwa.

Kamati ya Uchaguzi ya Simba ilitangaza kumuengua Wambura katika mchakato wa uchaguzi huo kutokana na kutokidhi sifa zilizoainishwa kwenye katiba.

Moja ya kosa linaloonekana kumuweka Wambura kwenye wakati mgumu ni hatua ya kuipeleka Simba mahakamani mwaka 2010 wakati katiba ya klabu hiyo, TFF na FIFA zote zinakataza kupeleka masuala ya soka kwenye mahakama za kawaida.

Kufuatia Wambura kuondolewa, sasa nafasi ya Urais imebaki na wagombea wawili ambao ni Evans Aveva kutoka Friends of Simba na Andrew Tupa wa Fans of Simba

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC