Ruka hadi kwenye maudhui makuu

KIPRE TCHETCHE WA AZAM FC NDIYE BORA LIGI KUU BARA

Mshambuliaji Kipre Tchetche wa mabingwa wapya Azam FC, ameibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu katika tuzo za wanasoka bora zilizotolewa usiku wa kuamkia jana na mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), kampuni ya huduma za mawasiliano ya Vodacom Tanzania.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast, alitwaa tuzo yake akiwapiku Anthony Matogolo wa Mbeya City na Lugano Mwangama wa Tanzania Prisons aliokuwa akichuana nao katika kipengele hicho.

Kwa tuzo hiyo, Kipre alizawadiwa Sh. milioni 5.2 ikiwa ni ongezeko la Sh. 200,000 ikilinganishwa na msimu wa 2013/14 wa ligi hiyo ambayo beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani aliinyakua.

Meneja wa Azam FC, Jemadari Said alipokea tuzo ya Tchetche kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.


Tchetche yuko kwao Ivory Coast kwa ajili ya mapumziko na wachezaji wote waliwakilishwa katika hafla hiyo kutokana na kuchelewa kutolewa kwa tuzo hizo tangu ligi hiyo imalizike Aprili 19 mwaka huu.

Katika tuzo hizo timu ya Yanga ilijipoza machungu ya kuvuliwa taji lake la ubingwa kwa kushinda tuzo ya Timu Yenye Nidhamu katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam ikishuhudia refa, kocha na wachezaji waliofanya vizuri msimu huu wakizawadiwa.

Yanga iliyokuwa imewakilishwa na mjumbe wa kamati ya utendaji, Salim Rupia, Kaimu Ofisa Habari, Baraka Kizuguto na Mhasibu Rose Msamila, ilikabidhiwa kombe na hundi ya Sh. milioni 16 na kampuni hiyo ikiwa ni ongezeko la shilingi milioni moja ikilinganishwa na zawadi ya msimu uliopita ambao Yanga pia waliichukua.

Yanga, ambayo iliiwakilisha pia Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika iliipiku Azam FC na JKT Oljoro zilizokuwa zikiwania pia tuzo hizo.

Aidha, kipa wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hussein Sharrif ‘Cassilas’ alishinda tuzo ya mlinda mlango bora wa msimu na kuzawadiwa Sh. milioni 5.2 akiwazidi kete Beno Kakolanya wa Tanzania Prisons na David Burhan wa Mbeya City aliyetwaa tuzo hiyo msimu uliopita akiwa na Tanzania Prisons ya Mbeya pia.

Juma Mwambusi wa Mbeya City alishinda tuzo kocha bora kutokana na kuiongoza vyema timu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya tatu, akiwaangusha Boniface Mkwasa wa Yanga na Mecky Mexime wa Mtibwa Sugar na kupewa Sh. milioni 7.8.

Zawadi ya Mwambusi ilichukuliwa na Emmanuel Kimbe, katibu wa Mbeya City kwa sababu kocha huyo yuko nchini Sudan na akikiongoza kikosi chake katika michuano mipya ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ya Nile Basin.

Kocha Abdallah 'King' Kibadeni wa Ashanti United alitwaa tuzo hiyo msimu uliopita akiwa na Kagera Sugar ambayo sasa inanolewa na Jackson Mayanja.

Refa Israel Nkongo wa Dar es Salaam aliibuka mwamuzi bora akilamba Sh. milioni 7.8 baada ya kuwabwaga Isihaka Shirikisho wa Tanga na Jonasia Rukya wa Kagera walioingia kwenye kipengele hicho.

Msimu uliopita tuzo hiyo ilikwenda kwa Simon Mbelwa wa Pwani na msimu wa 2011/12 ilichukuliwa na 'afande' Martin Saanya wa Morogoro.

Tuzo ya mfungaji bora wa msimu ilikwenda kwa mshambuliaji wa Simba, Mrundi Amisi Tambwe, aliyefunga mabao 19 na kuzawadiwa Sh. milioni 5.2. Tuzo hiyo ilikuwa inawania pia na Tchetche aliyefunga magoli 13, Elias Maguli wa Ruvu Shooting (13), Mrisho Ngasa wa Yanga (12) na Hamis Kiiza wa Yanga pia (12).

Tchetche alinyakua tuzo hiyo msimu uliopita akifunga magoli 17, mawili nyuma ya straika na nahodha wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor' aliyetwaa tuzo hiyo msimu wa 2011/12.

Zawadi nyingine zilizotolewa ni pamoja na Sh. milioni 75 iliyokwenda kwa Azam FC waliotwaa ubingwa, Yanga SC walioshika nafasi ya pili Sh. milioni 35, Mbeya City Sh. milioni 26 katika nafasi a tatu na Simba waliokumbwa na migogoro na kujikuta wakimaliza nafasi ya nne walipewa Sh. 21.
Hapakuwa na tuzo kwa wachezaji bora chipukizi ambayo misimu miwili iliyopita zilitolewa. Viongozi wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na TFF waliokuwapo kwenye hafla hiyo hawakueleza sababu za kutotolewa kwa tuzo hizo.

Akizungumza kabla ya zoezi la kutoa tuzo hizo lililokuwa likirushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twisa alisema wamefurahishwa na ushindani ulioonyeshwa na timu 14 zilizoshiriki ligi hiyo msimu huu na kwamba wana mpango wa kuongeza mkataba wa kuidhamini.

Silas Mwakibinga, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TPLB, alizitaja changamoto zilizoikumba ligi hiyo msimu huu kuwa ni pamoja na miundombinu mibovu ya viwanja, ufinyu wa fedha za udhamini, migogoro ya klabu, ubovu wa marefa, hujuma za mapato kwa kutotumika kwa tiketi za elektroniki, fujo na uhuni wa mashabiki viwanjani.

Alisema Ligi Kuu msimu huu iliangaliwa na watu 728,600 waliokata tiketi ikilinganishwa na watu 652,089 wa msimu uliopita.

Mgeni rasmi (Malinzi) alizipongeza kampuni za Vodacom Tanzania na Azam Media kwa kudhamini ligi hiyo huku akiweka wazi kwamba muda wowote wataanza mazungumzo na uongozi Vodacom Tanzania ili waingie nao mkataba mpya.

Mkataba wa miaka mitatu wa kampuni hiyo na TFF utamalizika msimu ujao na tayari shirikisho hilo limeshatangaza kuwa kuanzia msimu wa 2015/16 ligi hiyo itakuwa ikishirikisha timu 16.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC