Ruka hadi kwenye maudhui makuu

NCHI YASIMAMA KUMZIKA GURUMO LEO

Wakati Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanamuziki Muhidin Gurumo 'Mjomba', mwili wa gwiji huyo wa muziki wa dansi nchini unatarajiwa kuagwa rasmi leo kuanzia saa 2 asubuhi kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwao Masaki kwa ajili ya maziko yatakayofanyika mchana.


Awali ilipangwa marehemu Gurumo aliyefariki juzi katika hospitali ya Muhimbili azikwe jana, lakini atazikwa leo kwa kuzingatia wosia ulioachwa na kusisitizwa na gwiji huyo enzi za uhai kuwa asiharakishwe kuzikwa mapema na familia imeamua kutii wosia huo.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu Gurumo, Mabibo External, Msemaji wa familia, Yahya Mikole alisema mara kadhaa Mzee Gurumo alikuwa akiwasisitiza kuwa atakapokufa asizikwe kwa haraka.

Mikole ambaye ni binamu wa marehemu alisema, Mzee Gurumo alikuwa akimwambia kwa kuwa yeye ni mwanamuziki mkubwa na maarufu hivyo kuharakishwa kuzikwa kwake kunaweza kuwanyima wengine kumuaga au kuhudhuria maziko yake.

"Kwa kuzingatia hilo na ombi kutoka serikalini, tumeamua kusogeza shughuli za mazishi ya merehemu kutoka leo (jana) mpaka kesho (leo) na utaratibu wa kuaga utaanza saa 2-4 asubuhi kabla ya msafara kuondoka kwenda kumpumzisha kijijini kwao majira ya saa 7 mchana," alisema Mikole.

Msemaji huyo alieleza marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la mapafu na ugonjwa wa moyo na juzi kabla ya kifo chake alipatwa na tatizo la ukosefu wa damu na alipofikishwa Muhimbili aliwekewa chupa tatu za damu.

"Tatizo la ukosefu wa damu lilijitokeza juzi na aliwekewa chupa tatu zilizoisha asubuhi ya juzi kabla ya alasiri kupoteza maisha, huku akionekana mwenye afya yake ya kawaida kabisa," alisema Mikole.

Mikole alisema taratibu za mazishi ya marehemu zinaendelea kama kawaida nyumbani kwa marehemu.

Kwenye msiba huo watu mbalimbali wakiwamo wanamuziki wa zamani na walio wahi kufanya kazi na marehemu walihudhuria kama akina Juma Ubao, Mjushi Shemboza, Karama Regesu na wengine.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha mwanamuziki huyo maarufu na wa siku nyingi kilichotokea juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua kwa muda mrefu.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Muhidini Mwalimu Gurumo ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia taifa hili kwa bidii tangu miaka ya '60 kupitia sanaa ya muziki katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi kuanzia bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake.

Rais Kikwete alisema mchango wa marehemu Gurumo kwa taifa letu ni mkubwa na wa kupigiwa mfano kupitia kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu ambacho alikitumia kikamilifu kwa manufaa ya wananchi wa nchi yetu na taifa kwa ujumla.

Rais Kikwete alimuomba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Gurumo kwa kumpoteza kiongozi na mhimili wa familia yao. Alisema binafsi anaungana na familia ya marehemu kuomboleza msiba huo mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi roho ya marehemu, Amina.

Aidha, Rais Kikwete aliwaomba wanafamilia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa mpendwa wao kwa kutambua kwamba yote ni mapenzi yake Mola.

Naye kocha maarufu wa soka na mdau mkubwa wa bendi ya Msondo Ngoma, Jamhuri Kihwelu 'Julio' amemlilia Gurumo akidai kifo chake ni pigo kwa familia, wadau wa muziki na michezo nchini.

Julio aliyewahi kuichezea na kuinoa Simba kabla ya kutua Mwadui-Shinyanga na kukaribia kuipandisha Ligi Kuu, alisema kifo cha Gurumo kwake ni pigo kubwa kwani alikuwa ni mjomba wake mbali na unazi wao wa Simba na Msondo.

Alisema yeye binafsi ameumia sana kwa msiba wa mwanamuziki na mwanachama huyo wa Simba kama ambavyo wadau wa fani za muziki na michezo walivyoumizwa na kudai ni vigumu kupatikana wa kuziba pengo lake.

"Kwa hakika nimeumia kama walivyoumia wadau wa michezo na muziki kwani enzi za uhai wake, Gurumo alikuwa mwanachama wa Simba na pia ni gwiji wa muziki ambaye hakuwa na mfano wake katika kizazi chake," alisema Julio.

Julio, alisema marehemu Gurumo alikuwa mmoja wa watu wa mfano kwa kule kuipenda fani yake na kujali masilahi ya wanamuziki, mbali na kufanya kazi kwa umri mkubwa mpaka miezi michache alipotangaza kustaafu.

Alisema kustaafu na mwisho kufa kwake, kumeifanya safu ya mbele ya Msongo kutoweka baada ya kuondoka kwa Tx Moshi, Joseph Maina, Athuman Momba na Suleiman Mbwembwe.

"Itatuchukua muda mrefu kumsahau Mzee Gurumo, nakumbuka wakati anaumwa mara kwa mara nilikuwa namtembelea kumjulia hali na kutaniana naye sijui nitamtania nani tena, kwa kweli naumia..Mungu amrehemu," alisema Julio.Enzi za uhai wake Gurumo alikuwa mwanachama wa Simba na shabiki mkubwa wa mabingwa watetezi wa England, Manchester United.

Chini ya uongozi wa akina Hassan Dalali, Mzee Gurumo aliwahi kuwapelekea wachezaji wa Simba wakiwa mazoezi matunda mbalimbali kutoka shambani mwake kwa nia ya kuboresha siha na afya zao kuonyesha unazi wake wa Simba.

Nalo Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa gwiji huyo.

Katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mtendaji BASATA, Godfrey Mngereza, baraza hilo limestushwa ma msiba huo.

“Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Muhidini Mwalimu Gurumo ambaye mchango wake katika muziki wa dansi ni mkubwa mno na ulikuwa unahitajika sana, pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wake bado unahitajika katika tasnia hii. Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini.

Aidha tunawatakia moyo wa subira wote katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.

"Mwenyezi Mungu aipumzishe mahala pema peponi roho ya marehemu. Baraza liko pamoja na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi."

Marehemu Gurumo aliyezaliwa mwaka 1940 ameacha mjane mmoja na watoto sita, watatu wa kiume ambao ni Abdallah, Omar na Mwalimu na wa kike pia wakiwa watatu ambao ni Mariam, ambaye ndiye mtoto mkubwa wa marehemu, Mwazani na Kibibi aliye wa mwisho kuzaliwa.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC