Ruka hadi kwenye maudhui makuu

YANGA YAFUFUA MATUMAINI YA UBINGWA

MABINGWA watetezi, Yanga SC jana wamezinduka baada ya kuwachapa mabao mawili 3-0 wenyeji Rhino Rangers katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabira.

Shujaa wa Yanga SC, jana alikuwa ni mshambuliaji Jerry Tegete aliyefunga mabao mawili moja kila kipindi, wakati lingine lilifungwa na Hussein Javu kipindi cha pili.

Yanga SC sasa inatimiza pointi 43 baada ya mechi 20 na kuendelea kubaki nafasi ya pili, nyuma ya Azam FC yenye pointi 44 baada ya kucheza mechi 20 pia.

Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm alifanya mabadiliko katika safu yake ya ushambuliaji jana akiwaanzisha pamoja Mrisho Ngassa na Tegete badala ya Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza, wakati Emmanuel Okwi na Simon Msuva walikuwa wakishambulia kutokea pembezoni mwa Uwanja.
 
Tegete aliifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya 30 kwa shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Charles Mpinuki kufuatia mchomo mkali wa kiungo Hassan Dilunga.


Kipa Juma Kaseja aliokoa michomo ya hatari ya Rhino katika dakika za 27, 42 na 45, wakati Dilunga mbali na shuti lililorudishwa na kipa kabla ya kujazwa nyavuni na Tegete, pia aligongesha mwamba mara mbili dakika za 20 na 26.
 
Kipindi cha pili, Yanga SC waliendelea kulishambulia lango la Rhino na dakika ya 69, Tegete tena alifunga bao la pili baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa timu hiyo ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kufuatia krosi ya winga Simon Msuva. Mpira huo ulimparaza beki Laban Kambole wakati unatinga nyavuni.

Hussein Javu aliyetokea benchi dakika ya 79 kuchukua nafasi ya Tegete, aliifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 90 akiitendea haki pasi nzuri ya Okwi nje kidogo ya lango la Rhino.

Huu unakuwa ushindi wa kwanza kwa Yanga SC ndani ya mechi tatu za Ligi Kuu, baada ya kulazimishwa sare mbili mfululizo na Mtibwa Sugar 0-0 mjini Morogoro na Azam FC 1-1 mjini Dar es Salaam, mechi zote wapinzani wake wakiwa pungufu ya mchezo mmoja baada ya kadi nyekundu.
 
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Jerry Tegete/Hussein Javu dk79, Mrisho Ngassa na Emmanuel Okwi.
 
Rhino Rangers; Charles Mpinuki, Julius Masunga, Ally Mwanyiro, Abdallah Said, Laban Kambole, Msafiri Hamisi, Hussein Abdallah, Mussa Digubike, Gideon Brown, Rajab Twaha na Suleiman Jingo/Abbas Mohammed dk79.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo jana, JKT Ruvu  imefungwa mabao 2-0 na Mbeya City  Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam, mabao yote yakitiwa kimiani na Saad Kipanga dakika za tisa na 69. Mbeya City inatimiza pointi 42 baada ya mechi 22 na kuendelea kubaki nafasi ya tatu.

Ligi hiyo inaendelea leo kwa mechi nne, Simba SC wakimenyana na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Azam FC itaonyeshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex. Mechi hizo mbili zitakuwa ‘live’ kupitia Azam TV.

Mechi nyingine za leo ni Mgambo Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Ruvu Shooting na Ashanti United zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC