Ruka hadi kwenye maudhui makuu

YANGA YAFANYA KUFURU KWA PRISONS, YAITANDIKA 5-0

Mabingwa Yanga walirejea katika kasi yao ya kutoa vipigo vikali zaidi vya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu wakati walipobamiza Tanzania Prisons ya Mbeya kwa magoli 5-0, lakini ushindi huo haukutosha kuitingisha kileleni Azam ambayo nayo ilishinda 2-0 dhidi ya Mgambo mjini Tanga. 

Mabao ya Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa, Nadir Haroub 'Cannavaro' na mawili kutoka kwa mtokeabenchini, Hamis Kiiza yaliwapa Yanga ushindi mnono kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kujiimarisha katika nafasi ya pili ya msimamo wakiwa  na  pointi  46,  nne  nyuma  ya Azam.

Vinara Azam, ambao wamefikisha pointi 50 wakiwa wamecheza mechi moja zaidi ya Yanga, walipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Mkwakwani kupitia magoli ya John Bocco 'Adebayor' (dk.59), na Brian Umony (dk.82) na kujiweka katika mazingira mazuri kutwaa ubingwa wao wa kwanza katika historia zikiwa zimebaki mechi nne.
 

Kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga walipata goli la kwanza katika dakika ya 22 kupitia kwa Okwi aliyepiga shuti kali la chini la umbali wa mita takribani 26 wakati akipiga faulo iliyotolewa na refa Andrew Shamba kutoka Pwani baada ya beki na nahodha wa Prisons Lugano Mwangama kumkwatua raia huyo wa Uganda.

Prisons walipata fursa ya kusawazisha goli hilo katika dakika ya 35 wakati beki wa Yanga, Oscar Joshua alipocheza madhambi ndani ya boksi na kuzaa penalti ambayo Mwangama alipaisha mbele ya kipa Juma Kaseja ambaye alikuwa tayari amepotea langoni.

Katika tukio hilo, nahodha wa Yanga, Cannavaro alionywa kwa kadi ya njano kwa kupinga maamuzi ya refa.

Yanga walipata goli la pili katika dakika ya 38 kufuatia shambulizi kali la kushtukiza kupitia kwa mshambuliaji mtokeabenchini Hussein Javu aliyekimbia na mpira kutoka katikati ya uwanja na kumimina krosi murua iliyomkuta winga Ngasa akiwa peke yake na akautumbukiza mpira nyavuni.

Kiiza, ambaye aliingia katika dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Okwi ambaye aliumia tumbo na kutolewa kwa machela, aliiandikia Yanga bao la tatu katika dakika ya 68 akiitendea haki krosi safi ya ndani ya sita kutoka kwa Simon Msuva iliyoshuhudia mpira ukimpita ubavuni kipa kabla ya kumfikia Mganda huyo.

Mapishi ya goli hilo yalianzia katika kazi hiyo iliyofanywa na kiungo Hassan Dilunga katikati ya uwanja kabla ya kutoa pasi kwa Msuva pembeni Kaskazini Magharibi mwa lango la Kaskazini mwa Uwanja wa Taifa.

Cannavaro aliipatia Yanga goli la nne kwa njia ya penalti katika dakika ya 78 kufuatia Hussein Javu kufanyiwa faulo kwenye mstari wa boksi na Kiiza akafunga goli lake la pili jana na la tano kwa Yanga katika dakiia ya 88 akimalizia krosi kali ya Javu, ambaye kuingia kwake kuliubadili kabisa mchezo huo.

Kocha wa Prisons, David Mwamaja alisema baada ya mechi hiyo: "Kukosa penalti kulituathiri. Tungepata penalti ile tungekuwa na uwezo wa kupata matokeo mazuri. Kipa pia hakuwa vizuri katika baadhi ya mashambulizi. Kukosekana kwa Omega Seme kumetuathiri. Tutakuwa na usongo wa mechi ijayo."

Naye kocha wa Yanga, Mholanzi, Hans van der Pluijm alisema: "Vijana wamecheza kwa mbinu zetu za Kidachi. Ni ushindi mkubwa kwetu na unatuimarisha kuendelea kupambana."

Kulikuwa na watazamaji wachache waliokuwa wameingia Uwanja wa Taifa kutazama mechi hiyo ikiwa ni mwendelezo wa mwenendo mbaya wa mapato ya mlangoni kwa klabu ya Yanga tangu itolewe kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly na kisha kutoa sare mbili mfululizo dhidi ya Mtibwa na Azam FC.

Klabu hiyo ya Jangwani pia itaendelea kutoambulia chochote katika mapato ya mlangoni hadi pale Sh. milioni 106 za wachezaji wake wa zamani Stephen Malashi na Wisdom Ndhlovu zitakapokamilika kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi).

Tayari Shirikisho la Soka (TFF) limeanza kuikata klabu hiyo wakichukua Sh. milioni 9.2 za mgawo wa mapato ya Sh. milioni 38.6 za mechi yao iliyopita dhidi ya Rhino Rangers kulipa deni hilo lililotokana na wachezaji hao kukatishiwa mikataba yao.

Vikosi vilikuwa: Yanga: Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Jeryson Tegete/ Hussein Javu (dk 34), Mrisho Ngasa/ Haruna Niyonzima (dk.75) na Emmanuel Okwi/ Hamis Kiiza (dk 60) .

Tanzania Prisons: Beno Kakolanya, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, Lugano Mwangama, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Godfrey Mageta/ Jimy Shoji (dk.68), Fred Chundu, Peter Michael, Frank Hau na Ibrahim Mamba/ Six Mwakesaga (dk.49).

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC