
Wachezaji wa Arsenal Alex
Oxlade-Chamberlain na Kieran Gibbs wameondolewa adhabu ya kadi nyekundu
baada ya Gibbs kuondolewa uwanjani kimakosa wakati wa mchuano wa siku ya
Jumamosi ambapo Arsenal ilishindwa vibaya na Chelsea kwa kipigo cha
magoli 6-0 uwanjani Stamford Bridge.
Jopo la chama cha soka England, FA, limesema
kuwa refa Andre Marriner alikosea kwa kumtimua uwanjani Kieran Gibbs na
kwamba tukio la Oxlade-Chamberlain kuunawa mpira katika eneo la hatari
haikustahili kadi nyekundu.
Sasa wachezaji hao hawatahudumia marufuku ya mechi kutokana na tukio hilo.
Maafisa wa usimamizi wa mechi walisema kuwa refa
huyo mwenye umri wa miaka 43, ambaye tayari ameomba msamaha kwa
kukanganya majina ya wachezaji, anapaswa kupewa fursa nyingine
kurekebisha makosa yake badala ya kunyimwa kibarua mwishoni mwa juma
hili.