Ruka hadi kwenye maudhui makuu

RAGE AMFUNIKA HANSPOPE UWANJA WA NDEGE, ATAMBA YEYE BADO MWENYEKITI SIMBA.

MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage aliwasili Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam jana usiku akitokea Sudan na kusema kwamba; “Mimi bado Mwenyekiti wa Simba SC,”.

Rage aliwasili kwa ndege ya shirika la Kenya saa 1:40 usiku na kutokea mlango wa Watu maalum (VIP) ambako alilakiwa na wanachama zaidi ya 200, waliokuwa kwenye mabasi sita aina ya Coaster.

“Umati huu uliokuja hapa ni kielelezo tosha sana kwamba kiasi gani wanachama wa Simba wana imani na Mwenyekiti wao, sasa leo sitasema mengi, nitakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari kesho saa saba mchana makao makuu ya klabu(Msimbazi),”alisema Rage.

Alipoulizwa kuhusu kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Jumatatu na kutangaza kumsimamisha, Rage alisema; “Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Kamati ya Utendaji haina uwezo wa kumsimamisha Mwenyekiti, usinimalizie utamu, njoo kesho mchana Msimbazi,”alisema.

Watu zaidi ya 200 walifika Uwanja wa ndege tangu saa 11 na ushei jioni ya jana kumsubiri Rage wakiimba nyimbo mbalimbali za kumbeza Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na kumpamba Rage huku wakicheza ngoma.


Na alipowasili walimlaki kwa shangwe na kucheza naye. Ilikuwa bonge la picha na waliofika kumlaki Rage walikuwa watu wa rika na jinsia tofauti, hadi wazee.

Rage baada ya kuzungumza kwa kifupi na Waandishi wa Habari alisema anaelekea makao makuu ya klabu, ambako wanachama wengine walikuwa huko wanamsubiri.

Jumanne wiki hii, Kinesi alisema, Kamati ya Utendaji ilimsimamisha Rage katika kikao chake cha Jumatatu usiku kwa sababu anaendesha klabu kwa kufanya maamuzi yake mwenyewe bila kushirikisha kamati ikiwemo kutoitisha vikao vya kamati ya utendaji kwa mujibu wa Ibara ya 31 (a).

Alisema sababu nyingine ni Rage kuahirisha mkutano Mkuu maalum wa katiba ulioidhinishwa na mkutano mkuu bila kuishirikisha kamati.

“Rage alisema mkutano usifanyike kwa sababu alikuwa na safari ya nje na kutaka matawi yaendelee kuleta taarifa za katiba, sisi tukaona kikatiba mkutano lazima uendelee kwani alikaidi,”alisema Kinesi.

Aidha, sababu nyingine ni mkataba wa kukiuza kipindi cha Simba Tv bila kuishirikisha kamati hiyo kinyume na ibara ya 30 (b) ya ibara ya katiba ilihali kamati hiyo na Mwenyekiti akiwa na taarifa ilikuwa na mazungumzo na Zuku Tv, kuuza kipindi hicho ambapo maongezi yalikuwa yamefikia Dola za Marekani 300,000 kwa mwaka pamoja na fungu la usajili kila mwaka ambalo lilikuwa bado halijajadiliwa.

Hata hivyo, Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, limesema halitambui uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji na kumuandikia barua Kinesi aliyeendesha kikao hicho kumtaka awape muhtasari wa kikao na pia aeleze wajumbe waliohudhuria.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Hamisi Kilomoni, alisema ingawa baraza bado halijajulishwa rasmi uamuzi wa kumsimamisha Rage, lakini wamekubaliana kwamba kuna makosa yalifanyika kwenye kikao hicho kulingana na katiba ya Simba, hivyo kutaka muhtasari huo kwa vile wao ndiyo wasimamizi wa masuala ya Simba.

“Kwanza mimi na mwenzangu Ramesh Patel (Mjumbe wa Baraza la Wadhamini) tumekubaliana kuna makosa yalifanyika kwenye kikao chao, hivyo uamuzi wao si sahihi. Tulichokifanya tumemuandikia barua Mwenyekiti aliyesimamia hicho kikao, atupe muhtasari wa kilichotokea na pia tufahamu wajumbe waliohudhuria.

“Sisi hawajatujulisha rasmi, badala yake nasi tumepata taarifa kutokana na vyombo vya habari, na kama unavyojua inawezekana kwenye vyombo vya habari kuna taarifa tofauti na yaliyojitokeza kwenye kikao…
“Hivyo ndiyo sababu tunataka muhtsari wa kikao ili kwanza tupate uhakika wa mambo, tujue walizungumza nini na masuala kama hayo.

Ila kama walijadili kama yanavyoelezwa kwenye magazeti, wamefanya makosa. Katiba haisemi hivyo, ” alisema Kilomoni ambaye amepata kuwa kiongozi wa Simba na pia mchezaji wa timu hiyo.

Wakati huo huo: Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe naye aliwasiri ndege moja na Rage, ingawa yeye ametokea, Lubumbashi, DRC alipokwenda kwa shughuli zake za kibiashara.

Hans Poppe, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) aliwavutia wanachama wa Simba SC alipotokea, lakini akawaomba hataki mapokezi, waendelee kumsubiri Rage.

“Msinipokee tafadhali, nawashukuru, msubirini Rage anakuja huko nyuma, nimemuacha ndani,”alisema.

Hans Poppe ni kipenzi cha wapenzi na wanachama wa Simba SC kutokana mchango wake mkubwa anautoa kwenye klabu hiyo wa hali na mali.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC