Ruka hadi kwenye maudhui makuu

YANGA YAACHANA NA NGASA............

Uwezekano wa winga wa Yanga, Mrisho Ngassa (Pichani) kuonekana Uwanja wa Taifa Jumamosi akiwa amevalia uzi wa kijani na njano wakati timu yake itakapokuwa ikivaana na Ruvu Shooting, sasa ni majaliwa baada ya klabu yake kususa kumlipia faini ya Sh. milioni 45 alizotakiwa kuilipa Simba.


Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, suala hilo kwa sasa haliko chini ya klabu yao, bali ni la Ngasa mwenyewe.

"Maamuzi yaliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), yanamtaka Ngassa na si klabu ya Yanga kulipa fedha hizo. Klabu ilikata rufaa kupinga maamuzi ya kumfungia mechi sita na si suala la kulipa fedha.

"Rufaa yetu tayari ilishatupwa na mchezaji amekosa mechi zote sita, hivyo hayo mengine ni juu yake," alisema Kizuguto.

Kwa upande wa TFF, ilisema Ngassa bado hajalipa fedha za Simba kama ilivyomtaka kutekeleza hilo kabla ya kumruhusu kuanza kuitumikia Yanga msimu huu.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema licha ya kukosa mechi sita ikiwamo ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Azam FC na tano za Ligi Kuu ya Bara msimu huu, Ngassa hajamaliza adhabu aliyotakiwa kuitumikia.

"Ngassa bado hajamaliza adhabu kwa kuwa hajalipa fedha za Simba. Mpaka sasa (jana saa 6:12 mchana) bado hajalipa fedha za Simba, hivyo haruhusiwi kucheza licha ya kwamba tayari ameshakosa mechi sita kama ilivyoamuliwa na kamati. Hawezi kucheza mechi ya Jumamosi kama hatalipa fedha hizo," alisema Osiah.

Kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilimpa Ngassa adhabu hiyo baada ya usajili wake kuleta utata kutokana na kujisajili klabu mbili tofauti, Simba na Yanga.

Hata hivyo, kamati hiyo ilitumia busara na kumwidhinisha Ngassa kuichezea Yanga msimu huu huku ikimtaka kuilipa Simba jumla ya Sh. milioni 45, kati ya hizo Sh. milioni 30 ni alizopewa kama ada ya usajili, wakati ambapo Sh. milioni 15 zikiwa ni asilimia 50  ya faini ya kiasi hicho cha fedha alichopokea.

Mbali na kutakiwa kulipa kiasi hicho, kamati hiyo ilimfungia kucheza mechi sita msimu huu. Kadhalika ilieleza wazi kwamba, Ngassa hataruhusiwa kuichezea Yanga kama atakuwa hajailipa Simba hata kama atamaliza kifungo cha kutocheza mechi sita.

NGASA

Kwa upande wa Ngassa ambaye aliwahi kuichezea Kagera Sugar, Azam FC na Simba, alipotafutwa jana kuzungumzia sakata hilo, kwanza alikataa kulitolea ufafanuzi kwa madai kuwa liko chini ya uongozi wa klabu yake ya sasa, Yanga.

"Waulize viongozi wa Yanga maana wao ndiyo walikuwa wanafuatilia suala hilo," alisema kwa kifupi mzaliwa huyo wa jijini Mwanza, huku akikataa kuendelea kuzunguza licha ya mwandishi wetu kumfahamisha kuwa Yanga imesema haihusiki na kulipa fedha hizo.

Agosti 23, mwaka huu Yanga iliwasilisha rufaa TFF kupinga maamuzi ya kumfungia winga huyo huku ikitishia kulipeleka suala hilo katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Hata hivyo, kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, shirikisho hilo liliitupa rufani hiyo ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kuwa haikubainisha kamati ya rufaa iliyolengwa na mrufani (Yanga).

"TFF ina kamati tatu za rufaa: kamati ya rufaa ya maadili, kamati ya rufaa ya nidhamu na kamati ya rufaa ya uchaguzi. Barua ya Yanga haikueleza rufaa yao ilitakiwa kupelekwa kwenye kamati ipi kati ya hizo tatu," alisema Wambura katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, maamuzi yanayotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji (iliyomhukumu Ngassa) ni ya mwisho nchini.

Ilielezwa kwamba kamati hiyo ilitumia busara badala ya kumhukumu Ngassa kwa mujibu wa Kanuni ya 44 (3) cha Kanuni za Ligi za TFF na Sura ya IV Ibara ya 17 (4) cha Kanuni za Fifa, ambapo winga huyo alitakiwa afungiwe kucheza soka kwa mwaka mzima huku klabu ya Simba ikistahili kifungo cha misimu miwili mfululizo pasipo kusajili wachezaji wa ndani na nje.

"Klabu inayomshawishi mchezaji kumsajili wakati akiwa na mkataba na timu nyingine kwa kusaini au kuvunja mkataba wake na klabu hiyo pasipo kuitaarifu klabu husika, itafungiwa na chama cha soka cha nchi husika kusajili wachezaji wa ndani na nje kwa misimu miwili mfululizo," inaeleza Sura ya Nne Ibara ya 17(3) cha Kanuni za Fifa.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC