Ruka hadi kwenye maudhui makuu

TAMBWE AZIDI KUTIKISA LIGI KUU

Mshambuliaji Amisi Tambwe (Pichani) jana alifunga goli lake la saba katika mechi tatu wakati alipoiongoza Simba kushinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.


Tambwe ambaye amejiunga na Simba katika kipindi kilichoisha cha usajili akitokea kuipa ubingwa wa Kombe la Kagame la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati timu ya Vital'O ya kwao Burundi, alifunga goli la kuongoza katika ya dakika 25 kwa penalti.

Simba ilipata penalti hiyo baada ya beki wa kati wa JKT Ruvu, Omar Mtaki kuonekana ameunawa mpira wa krosi iliyopigwa na haruna Chanongo. Refa wa kati hakuona kama kuna madhambi yamefanyika lakini mwamuzi wa pembeni John Kanyenye kuotoa Mbeya aliamua kuwa ni penalti.

Wachezaji wa JKT Ruvu waliilalamikia sana penalti hiyo huku mtunza vifaa wao, Selemani Oga, akiingia uwanjani kumzonga mwamuzi.

Hali hiyo iliendelea hata baada ya mechi hiyo kumalizika pale mchezaji Paul Ndauka alipoingia uwanjani kumzonga mwamuzi huyo ambaye alijaribu kumkwepa kwa kurudirudi nyuma.
Matokeo hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko.

Kipindi cha pili JKT Ruvu walirejea kwa kasi kwa nia ya kusawazisha goli hilo, lakini kushambulia mfululizo kuliwagharimu kwani walijikuta wakifungwa goli la pili kwa shambulizi la kustukiza.

Kiungo Abdulhalim Homoud alikimbia na mpira kutokea katikati ya uwanja kabla ya kupiga krosi iliyomkuta Ramadhan Singano 'Messi' aliyeusukumia mpira wavuni kwa mguu wa kulia, ikiwa ni dakika sita tu baada ya mapumziko. Messi alikuwa ameingia uwanjani katika dakika ya 36 kuchukua nafasi ya Amri Kiemba.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 14 kileleni baada ya mechi saba.

Katika mechi nyingine, Azam FC iling'ang'aniwa kwa sare ya 1-1 dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Wenyeji Prisons walitangulia kupata goli katika dakika ya 36 lililofungwa na Peter Michael kabla ya Azam kusawazisha kupitia kwa Kipre Tchetche katika dakika ya 49.

Kwenye Uwanja wa Azam Complex, timu inayoburuta mkia ya Ashanti United ilipata pointi yake ya pili tangu irejee kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Mtibwa Sugar. Ashanti ilipata magoli yake kupitia kwa Paul Maone na Tumba Swedi, wakati ya Mtibwa yalifungwa na Shaaban Kisiga.

Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa; Simba: Abbel Dhaira, Haruna Shamte, Adeyoum Seif, Kaze Gilbert, Joseph Owino, Abdulhalim Humoud, Amri Kiemba/ Ramadhani Singano (dk. 36), Said Ndemla, Betram Mombeki/ Miraj Madenge (dk. 73), Amisi Tambwe na Haroun Chanongo/Marcel Kaeza (dk. 57).

JKT Ruvu: Shaaban Dihile, Damas Makwaya, Stanley Nkomola, Omar Mtaki, Jamal Said, Nashon Naftali, Alhaj Zege, Emanuel Swita/ Richard Msenya (dk. 58), Bakari Kondo/ Paul Ndauka (dk.78), Salum Machaku na Emmanuel Pius.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC