OKWI KUREJEA ETOILE DU SAHEL, SIMBA ISUBIRI MAJALIWA........

SIMBA SC itaamua hatima ya msambuliaji wake wa zamani, Emmanuel Okwi (Pichani) mwishoni mwa mwezi huu kama itamrejesha au la, baada ya kufika kwa tarehe ya mwisho ya klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia iliyomnunua Januari mwaka huu ya kulipa fedha za manunuzi yake, dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh Milioni 480.


Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema juzi kwamba, Septemba 30 ndio wataamua wafanye nini baada ya kufika tarehe ya mwisho ya kulipwa fedha zao.

Kwa sasa, tayari Okwi, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda yupo Dar es Salaam akiwa amesusa kurejea Tunisia kutokana na madai ya klabu hiyo kushindwa kumlipa mishahara kwa miezi mitatu.

Okwi amekaririwa akisema kwamba tayari kesi yake ameifikisha Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), wakati Etoile nayo imekaririwa kudai imemshitaki mchezaji huyo FIFA pia kwa kushindwa kuripoti kazini kwa muda mrefu sasa, baada ya ruhusa ya kwenda kujiunga na timu yake ya taifa miezi miwili iliyopita.

Baada ya kumnunua mchezaji huyo Januari mwaka huu, Etoile iliahidi kutuma fedha za manunuzi yake mjini Dar es Salaam, lakini siku zilikatika hadi katikati ya mwaka, uongozi wa Simba ulipolazimika kwenda Tunis kufuatilia fedha hizo.

Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Hans Poppe aliongozana na Katibu wa klabu, Mwanasheria, Evodius Mtawala hadi Tunis na wakiwa huko, klabu hiyo iliahidi kulipa fedha hizo ifikapo Septemba 30.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI