Ruka hadi kwenye maudhui makuu

YANGA YAUMBUKA, VILABU LIGI KUU VYAWAKALIA KOONI

http://www.gushit.com/files/bookmark_photos/fdc9538552L.jpgSIKU moja baada ya uongozi wa Yanga kugomea haki za Ligi Kuu Tanzania Bara kuhodhiwa na Azam TV, uongozi wa Azam Media unaomiliki televisheni hiyo, umesema kujitoa kwa timu hiyo hakuna athari katika mchakato wa suala hilo ambalo limepokewa kwa furaha na klabu nyingine za ligi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa jana na kiongozi wa Azam TV, Saidi Mohamed, ikiwa ni siku moja tangu uongozi wa Yanga ugomee suala la haki za ligi hiyo kumilikiwa na Azam TV kwa hoja kuwa mchakato huo haukuwa wa uwazi na suala hilo lingefanyika baada ya uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania.

Yanga walikwenda mbali zaidi wakisema wao hawastahili kupata mgawo sawa na timu nyingine katika mkataba huo kutokana na kuchangia mapato makubwa tofauti na nyingine katika ligi hiyo, hivyo wanastahili kupata mgawo mkubwa zaidi na kuongeza kuwa kurusha mechi kutapunguza mapato.

Chini ya mkataba huo wenye thamani ya sh bil. 5.6 kwa kipindi cha miaka mitatu, kila klabu itapata kiasi cha sh mil. 25 kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Agosti 24 na baada ya kwisha kwa ligi hiyo, kila moja itapata sh mil. 75.

Akizungumzia tamko  la Yanga, Mohamed alisema kujitoa kwa Yanga katika suala hilo, hakutaaathiri mchakato wake wakiamini udhamini huo ni wenye tija kwa klabu za Ligi Kuu ambazo zimekuwa zikilemewa na gharama kubwa za uendeshaji.

Alisema kama Yanga watajitoa, hawataathiri uwepo wa udhami huo kwani watakachofanya ni kurusha mechi 13 za ugenini za timu hiyo na kuachana na mechi za nyumbani ambazo watakuwa na haki nazo kisheria.

“Kama kweli Yanga wataamua kujitoa, haina shida…. hatuwezi kuwalazimisha. Tutakachofanya ni kutorusha mechi ambazo wao watakuwa nyumbani, lakini zile za ugenini zitarushwa kama kawaida kwa mfano Shooting vs Yanga,” alisema Mohamed na kusema anaamini mpango huo ni ukombozi kwa timu nyingine za ligi hiyo na kuongeza: “Ligi Kuu ina timu 14….kama Yanga wataamua kujiweka kando na mkataba huo, bado hakutaathiri kitu maadamu kwa klabu zingine ni ukombozi mkubwa; tutakuwa hatuzitendei haki nyingine ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikilemewa na mzigo wa uendeshaji,” alisisitiza.

Wakati Yanga wakipinga udhamini huo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa klabu nyingi za Ligi Kuu zimeupokea kwa mikono miwili kwa hoja kuwa walau sasa zitapunguza matatizo kwani kiasi cha sh mil. 100, nje ya nauli na vifaa kutoka kwa mdhamini mkuu wa ligi hiyo, kampuni ya Vodacom, kutazipunguzia klabu makali ya ukata.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa klabu za Coastal Union, Ashant United na Ruvu Shooting, wametamka wazi kuwa mkataba huo ni ukombozi mkubwa sio kwao tu, bali kwa klabu zote za Ligi Kuu Soka Tanzania na kwenda mbali zaidi wakisema Yanga wana agenda yao binafsi.

Katibu Mkuu wa Ashant United iliyopanda daraja msimu huu, Abubakar Silas, alisema kiasi cha sh mil. 100 kwa kila klabu kwa msimu, ni ukombozi mkubwa kwa klabu kwani zitawasaidia kufanya mambo yao bila ya ubabaishaji, hivyo kuongeza hata ushindani wa soka uwanjani kutokana na ukweli kuwa ukata kuchangia timu kufanya vibaya.

“Ukweli ni kuwa Azam TV ni mkombozi wa soka la Tanzania. Naamini kwa udhamini huu, kwetu Ashant Utd tutafanya mambo makubwa katika ligi kwani haijawahi kutokea kila timu ikapata kiasi hicho cha fedha, umefika wakati sasa watu wakubali mabadiliko kama kweli tunataka kupiga hatua,” alisema Silas.

Naye ofisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema hofu kubwa ya Yanga, ni kuhofia changamoto kisoka kwani kila timu sasa itakuwa fiti kifedha tofauti na ilivyokuwa katika miaka iliyopita ambapo kwa kiasi kikubwa timu kubwa zilikuwa na unafuu mkubwa kupitia mapato ya milangoni na udhamini binafsi.

“Kitendo cha Azam TV kudhamini Ligi Kuu ni jambo la kupongezwa badala ya kukatishwa tamaa, hawa Yanga wanaonekana wana agenda yao ambayo haina nia njema na maendeleo ya soka ya Tanzania, kwani hoja zao hazina mashiko.

Naye Ofisa Habari wa Coastal Union, Edo Kumwembe, alisema wamepokea udhamini huo wa kihistoria ambao haujawahi kutokea katika soka ya Tanzania na kuongeza kuwa kama watu wataweka kando unafiki na kuzungumza ukweli, hata kama ungekuwa wa thamani ya sh mil. 50, bado ni wenye tija kwa klabu nyingi katika ligi hiyo.

“Tena huu ni mwanzo…hapo baadaye tunaweza kukaa kuuboresha zaidi, jamani kuna timu ambazo zimekuwa zikisajili kwa shida, achilia mbali sisi wenye udhamini wa Binslum, kuna timu zina ukata mkubwa, inaonekana wazi Yanga hawa wana jambo,” alisema Kumwembe.

Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema hawawezi kutoa kauli yoyote juu ya uamuzi wa Yanga kwani bado jambo hilo halijafikishwa kwao kimaandishi, lakini alionyesha kushangazwa na kali kuwa Yanga haikushirikishwa kwenye mchakato wa jambo hilo.

“Hatujapokea barua ya Yanga, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo baada ya kuona msingi wa madai. Lakini kwa hoja kuwa hawakuwa na mwakilishi, si kweli Katibu Mkuu Mwalusako (Laurance) na Makamu Mwenyekiti  Sanga (Clement) wameshiriki kubariki maamuzi,” alisema Wambura.

Kuhusu hoja kwa nini jambo hilo lisifanyike baada ya uchaguzi mkuu, Wambura alisema TFF iliamua kugawa majukumu yaliyoipa nguvu Kamati ya Ligi kukaa mezani kujadili udhamini huo chini ya dhama ya mgawanyo wa majukumu ambapo si shirikisho hilo kufanya kila kitu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC