Yanga kutembeza kombe mikoani

Baraka Kizuguto
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga watafanya  ziara ya mikoa kadhaa nchini kutembeza kombe lao la ubingwa wa ligi hiyo msimu uliopita kuanzia Julai 5, imeelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto alisema kikosi chao kinachonolewa na kocha Mholanzi Ernie Brandts kitatua jijini Mwanza Julai 5 kuanza ziara hiyo ambayo pia wataitumia kwa kucheza mechi za kirafiki kujiandaa kwa msimu ujao.

Kizuguto alisema wakiwa Kanda ya Ziwa, kikosi chao kitacheza mechi dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Uganda, timu ya Kampala City Council (KCC), Julai 6 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba (Mwanza), Julai 7 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na Julai 11 watavaana tena na Waganda hao kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

“Lengo la ziara hii ni kuwashukuru mashabiki kwa kuiunga mkono klabu na kupata mazoezi kabla ya msimu mpya,” alisema Frank Pangani, Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya Nationalwide, ambao ndiyo waandaaji wa ziara hiyo.

Msimu uliopita Yanga walitwaa ubingwa kwa kishindo baada ya kumaliza kileleni mwa msimamo wa mwisho wa ligi wakiwa na pointi 60, nne zaidi ya Azam waliowafuatia katika nfasai ya pili huku mahasimu wao wa jadi, Simba wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 45.