
Kanuni za usajili kama zilivyoainishwa na TFF,
inazitaka klabu kuhakikisha zinawapima afya wachezaji wapya
wanaowasajili kabla ya kuanza kucheza, jambo ambalo ni kinyume na timu
nyingi. Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema jana kuanzia mwaka ujao,
hakuna klabu itakayoruhusiwa kusajili wachezaji wapya bila kwanza
kuwapima afya na hiyo ni kwa mujibu wa kanuni.
Tenga alisema kanuni ziko wazi kwamba, mchezaji ni
lazima apimwe afya kabla ya kusajiliwa, na hii iko kila sehemu mchezo
wa soka unakochezwa kwa kiwango cha juu.
“Kuanzia mwaka ujao, TFF haitapokea mikataba ya
usajili wa wachezaji ambayo haitaambatana na taarifa za afya ya
mchezaji baada ya kupimwa na klabu anayokwenda kujiunga.
“Kupima afya ya mchezaji kabla ya kumsainisha
mkataba ni suala la kikanuni, siyo suala la hiyari na TFF kwa upande
wake itahakikisha zoezi hilo linafanyika,” alisema Tenga.
“Kuna mambo mengi yanafanyika kiholela, TFF
imejitahidi kwa uwezo wake kuyashughulikia kama msimamizi wa soka,”
alisema. Aliongeza: “Tumeanza kutekeleza kwa vitendo kanuni moja baada
ya nyingine na ndiyo maana msimu uliopita tulizibana klabu kuhusu timu B
kucheza ligi na hilo lilifanyika.
“Tunafahamu kuna ugumu, hayawezi kutekelezeka yote
kwa mara moja lakini tunamaliza moja na kuchukua lingine hadi mpaka
tutakapoona klabu zinaendeshwa kisasa.”
Akizungumzia suala hilo, Meneja Wa Azam FC,
Patrick Kahemele alisema kwa utaratibu wa klabu yao ni lazima wachezaji
wa wageni wapimwe afya zao kabla ya kusajiliwa ndani ya timu.
“Hatujawahi kusajili mchezaji bila kumpima afya,
labda awe mchezaji wa ndani ya timu kwa maana ya kumpandisha daraja kwa
sababu wao tayari wanakuwa wamepimwa,” alisema Kahemele.