SIMBA YALIPIZA KISASI YANGA, YAFANYA USAJILI KIMAFIA

Wakati uongozi wa klabu ya Yanga ukiwa katika harakati za kutaka kumsajili Mganda Moses Oloya anayecheza soka nchini Vietnam, uongozi wa Simba ambayo pia inamuwania mshambuliaji huyo umesema utawapiga bao watani wa jadi wao hao.

Akizungumza  kwa njia ya simu akiwa Nairobi, Kenya Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema jana kuwa wanajua kuwa Yanga wanamfuatilia mchezaji huyo lakini hawatishiki.
Alisema hawatishiki kwa kuwa wamefikia hatua nzuri ya mzungumzo na mchezaji huyo anayemalizia mkataba wake kwenye klabu yake ya huko Vietnam.
Hanspope alisema Simba haishindani na timu yoyote katika usajili na kwamba inafuata matakwa ya benchi la ufundi.
"Ni kweli sisi tunamfuatilia huyo mchezaji na bado tupo naye kwenye mazungumzo ila kwa kiasi kikubwa tumekubaliana vitu vingi," alisema mwenyekiti huyo.
"Kwa sasa kuna jambo moja tu tunalolisubiri ili kukamilisha taratibu zote."
Yanga imezoea kuingilia kati kila usajili unaofanywa na Simba, alisema Hanspope, lakini safari hii timu yake ipo makini kutorudia makosa waliyoyafanya msimu uliopita.
Simba iliporwa beki Mbuyu Twite wa APR wakati huo licha ya kuwa ya kwanza kufanya naye mazungumzo, na mwenyekiti Isamil Aden Rage kupiga naye picha nchini Rwanda, baada ya Yanga kwenda kwa klabu mama ya mchezaji huyo ya FC Lupopo ya JK Kongo.
Alisema kuwa suala la usajili wa Oloya wanaliendesha kwa umakini mkubwa kwa kuwa wanafahamu wenzao wanaweza wakawatibulia na kushindwa kukamilisha usajili huo.
Wakati Hanspope akisema hivyo, Yanga wanaendelea kusaka mchezaji mmoja wa kimataifa na taarifa zilizopo ni kuwa yupo kiongozi aliyekwenda Vietnam kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kumalizana na mchezaji huyo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya klabu hiyo Abdallah bin Kleb alikataa kuzungumzia jambo hilo na kusema,
"Sitaki kuzungumzia jambo hilo kwa sasa mpaka hapo mambo yatakapokamilika ila tunatafuta mshambuliaji mmoja wa kimataifa," alisema bin Kleb.