Ziara hiyo iliyodhaminiwa na kampuni ya bia ya TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro, ilijumuisha wanamuziki mchanganyiko kama Judith Wambura, Linex Sunday, Roma Mkatoliki, Ommy Dimpoz, Kala Jeremiah, Profesa Jay na mkali wa muziki wa R&B nchini Ben Pol.
Wanamuziki waliotia fora katika tamasha hilo ambalo wiki ijayo
linatarajia kuelekea katika mkoa wa Tanga ni Ben Pol ambaye alikuwa wa
pili kupanda jukwaani. Mashabiki walionekana dhahiri kumuelewa na
kuitikia kila wimbo aliokuwa akiimba na kusababisha wakati mwingine yeye
kukaa kimya na kuachia mashabiki hao waimbe mwanzo hadi mwisho wa
wimbo.
Ben Pol alipanda na wimbo 'Maneno Maneno' na kusababisha shangwe
kubwa uwanjani, na baada ya hapo, aliimba nyimbo zake maarufu kama
'Pete', 'Jikubali', 'Samboira', 'Nikikupata' na 'Maumivu'.
Lady Jaydee alikuwa ni mwanamuziki mwingine aliyeshangiliwa sana,
baada ya kupanda jukwaani akiwa bila bendi, jukwaa ambalo aliacha
kupanda kwa takriban miaka saba sasa, mara baada ya kuanzisha bendi yake
ya Machozi.
Jaydee alipanda jukwaani na wimbo aliomshirikisha marehemu Albert
Mangweha, ambapo baada ya kumaliza alisema ni heshima yake kwa kijana
huyo ambaye ameacha alama katika muziki wa kizazi kipya nchini. Baada ya
hapo aliendelea na vibao kama 'Wangu', ambapo alikuwa akiimba na kurap
mwenyewe, hali iliyosababisha uwanja mzima wa Jamhuri kushangilia muda
wote aliokuwa akiimba.
Ulipofikia wakati wa kuimba wimbo wa 'Joto Hasira', akasindikizwa
na Profesa Jay ambaye alizidi kupagawisha maelfu ya wakazi wa Dodoma
waliokuwa wamefurika uwanjani hapo kuangalia uzinduzi wa ziara hiyo ya
muziki ya Kili ambayo mwaka huu haijumuishi washindi wa tuzo kama ilivyo
kawaida, bali wasanii wanaong'ara katika medani ya muziki wa kizazi
kipya.
Akiongea baada ya onesho hilo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, ambaye
alionekana kufurahia onyesho alifafanua kwamba kampuni yake, kupitia
bia ya Kilimanjaro imedhamiria kuupeleka muziki wa Tanzania katika hadhi
yake na ndio maana mwaka huu, imebeba mandhari ya kikwetukwetu, ili
kuipa sanaa ya Kitanzania nafasi ya kutambulika.