MABINGWA
wa dunia, Hispania wametinga Nusu Fainali ya Kombe la Mabara kufuatia
ushindi wa mabao wa 3-0 dhidi ya Nigeria usiku huu.
Bao maridadi la juhudi binafsi za Jordi
Alba, mmoja kati ya wachezaji wanane wa Barcelona kwenye kikosi cha
kwanza cha Hispania, liliiweka Hispania mbele mbele baada ya dakika
tatu, kabla ya Fernando Torres kufunga bao lake la tano kwenye
mashindano haya dakika ya 62 kwa kichwa cha mkizi, dakika tatu tu
aingine aingie kuchukua nafasi ya Roberto Soldado.
Pamoja
na kufungwa, Super Eagles walicheza vizuri na kilichowagharimu ni
umaliziaji mbovu. Alba akafunga bao la tatu kwa Hispani na la pili kwake
katika mchezo huo dakika ya 88.Matokeo hayo yanaifanya Hispania iongoze Kundi B kwa pointi zake tisa na itakutana na Italia waliowachapa 4-0 katika fainali ya mwaka jana ya Euro 2012 kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mabara Alhamisi mjini Fortaleza.
Katika Nusu Fainali nyingine, Uruguay iliyoifunga 8-0 Tahiti usiku huu, imeshika nafasi ya pili kwenye Kundi hilo na itamenyana na Brazil katika Nusu Fainali. Nigeria baada ya kufungwa imemaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi zake tatu ilizovuna kwa vibonde Tahiti.