
Bendi ya FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma
Bendi ya FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma' wamealikwa kutumbuiza katika kinyang'anyiro cha kumsaka kinara wa shindano la kumsaka Miss Redd’s Kanada ya Nyanda za Juu Kusini kitakachofanyika Soweto mjini Mbeya kesho.
Shindano hilo la Nyanda za Juu ni miongoni mwa mashindano 10 ya kuwasaka vinara wa shindano la Miss Redd's ngazi ya kanda yatakayofanyika mwishoni wiki hii katika maeneo mbalimbali nchini, baadhi yakiwa ni ya kuwasaka washindi wa shindano hilo kanda za Mashariki na Ziwa.
Taarifa kutoka kwa waandaaji wa mashindano hayo zilieleza jana kuwa keshokutwa, kinyang'anyiro hicho kitakuwa mjini Morogoro wakati warembo kibao watakapopanda jukwaani kuwania taji la Miss Redd’s Kanda ya Mashariki. Watasindikizwa na kundi la msanii Wanne Star.
Taarifa hiyo imeeleza zaidi kuwa keshokutwa hiyo hiyo kutakuwa pia na shindano la kumsaka Miss Redd’s Kanda ya Ziwa litakalofanyika jijini Mwanza na kusindikizwa na burudani kadhaa zikiwamo za wakali wa muziki wa kizazi kipya, Ommy Dimpoz na Michael.
Mshindi katika Shindano la Redd’s Miss Tanzania linalodhaminiwa na kinywaji cha Redd’s kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ndiye atakayeiwakilisha Tanzania katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia.