Mwenyekiti wa kamati ya usajili Hanspope
Na Pasko Linda
WACHEZAJI watatu wa klabu bingwa ya Angola, Recreativo de Libolo watajiunga na Simba SC kwa mkopo mwishoni mwa msimu, imeelezwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia mambouwanjani.blogspot.com
jana kwamba, Libolo imekubali kuipatia klabu yake wachezaji hao watatu.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), hakuwa tayari kutaja majina ya wachezaji hao, lakini alisema ni beki wa kati mmoja, kiungo na mshambuliaji.
“Sisi tumezungumza na Libolo, wamesema watatupa kwa mkopo hao wachezaji, kwa kuwa hivi sasa tuna wachezaji watatu wa kigeni, tutaangalia namna gani tufanye ili tuwe na wachezaji wa tano kwa mujibu wa kanuni,”alisema Poppe.
Kwa sasa Simba SC ina Waganda wawili, Abbel Dhaira na Mussa Mudde na mshambuliaji Mzambia, Felix Sunzu. Beki Komabil Keita wa Mali amejitoa kwenye timu hiyo.
Simba SC ilitolewa na Libolo katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 5-0, ikifungwa 1-0 Dar es Salaam na 4-0 Angola.
Libolo imeonyesha ni timu nzuri kwa kufanikiwa kusonga mbele hadi kufika hatua ya makundi, baada ya mwishoni mwa wiki kuifunga Enugu Rangers na Nigeria mabao 3-1 Jumamosi.
Katika mchezo wa kwanza ugenini nchini Nigeria, Libolo ililazimisha sare ya bila kufungana.
Libolo wameingia katika uhusiano mzuri na Simba SC ambao unaonekana utainufaisha zaidi timu ya Tanzania, kwa kuanzia ni kupatiwa wachezaji hao watatu.