AZAM YAMALIZANA NA STRAIKA WAKE

Klabu ya Azam imemwongezea mkataba mshambuliaji wao wa kimataifa kutoka Kenya, Humprey Mieno baada ya kumaliza kuitumikia klabu hiyo kwa mkopo akitokea Sofapaka ya Kenya.

Mieno ambaye alionyesha kiwango kizuri wakati wa Ligi Kuu na kuifanya Azam kubaki katika nafasi ya pili, kulimfanya kocha wa Azam kuuomba uongozi kumpatia mkataba mchezaji huyo.
Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa, alithibitisha kumalizika kwa makubaliano kati ya mchezaji na uongozi wa Azam na kufikia mwafaka.
“Mieno alikuwa mmoja wa wachezaji waliomaliza mkataba, lakini kocha pamoja na uongozi umeona ni vyema ukampa muda zaidi kwani ameonyesha kiwango kizuri,”alisema kiongozi huyo.
Kwa upande wa rais wa Sofapaka Elly Kalekwa, alisema kiungo huyo amefikia mwafaka na klabu ya Azam baada ya kumwongezea mkataba na wao tayari wamepokea barua ya makubaliano.
Kalekwa alisema Mieno ameonyesha uwezo mkubwa ndani ya kikosi cha Azam ndiyo sababu iliyosababisha kuongezewa mkataba.
“Hatutakuwa na Mieno tena baada ya Azam kumwongezea mkataba, na sisi kama viongozi wake tunamtakia heri na mafanikio katika kazi,”alisema Kalekwa.