Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutogombea ubunge Ruangwa

Taarifa rasmi zinaeleza kuwa, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa hatogombea tena ubunge wa Ruangwa, Mkoa wa Lindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.

Dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu CCM za udiwani na ubunge lilifunguliwa kuanzia Juni 28, 2025 na linatarajia kufungwa leo jioni saa 10:00.

Uamuzi wa Majaliwa umetangazwa leo Jumatano na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi, Abbas Makwetta:

“Mheshimiwa Majaliwa amekuja na kusema hagombei tena ubunge.”

Ikumbukwe hivi karibuni akiwa Bungeni, Waziri Mkuu alitangaza kuwa atagombea jimbo hilo hivyo kwa uamuzi huu, atakuwa ameahirisha uamuzi wake wa awali.

Majaliwa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Tanzania amekuwa Mbunge wa Ruangwa kwa miaka 15 mfululizo kuanzia mwaka 2010.

Majaliwa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu katika utawala wa awamu ya tano chini ya Hayati Dkt. John Magufuli.