Wallace Karia hana mpinzani TFF

WAGOMBEA wote wa nafasi ya Urais Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wameenguliwa na aliyepitishwa na mtetezi wa nafasi hiyo pekee, Wallace John Karia kuelekea uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 16, mwaka huu Jijini Tanga.

Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Kiomoni Kibamba imewataja wagombea walioenguliwa kuwania Urais kwa vigezo mbalimbali vinavyomaanisha kukosa sifa ni pamoja na Mwenyekiti wa zanani wa klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Mbette Msolla, ambaye pia amewahi kuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars.

Wagombea wengine walioenguliwa ni Ally Thabit Mbingo, Mustafa Salum Himba, Shijja Richard na kiungo wa zamani wa Kimataifa wa Tanzania, Ally Mayay Tembele aliyechezea pia klabu ya Yanga.

Katika wagombea wa nafasi sita za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji waliopitishwa ni 10 pekee kati ya 19 waliojitokeza ambao ni Hossea Hopaje Lugano, Cyprian Charles Kuyava, Evance Gerald Mgeusa, Issa Mrisho Bukuku, James Patrick Mhagama, Khalid Abdallah Mohamed, Lameck Nyambaya, Mohamed Omar Aden, Salum Ally Kulunge na Vedastus Kalwizira Lufano.

Walioenguliwa ni Ally Omar Msigwa, Dk. David Cleopa Msuya, Dk. Yono Stanley Kevela, Juvenalius Pius Rugambwa, Maanya Juma Maanya, Martin Kibua Sekisasa,, Robert Bundala Kajuba, Rocky Raymond Mgeju na Saleh Alawi Abdullah.

Wagombea wa Urais walichukua fomu kwa gharama ya Sh. 500,000 kila mmoja, wakati nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji Fomu zimetolewa kwa gharam ya Sh 200,000.