Twiga Stars yatupwa nje WAFCON

TIMU ya Tanznaia imetolewa katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) baada ya kuchapwa mabao 4-1 na Ghana usiku wa Jumatatu katika mchezo wa mwisho wa Kundi C Uwanja wa Manispaa ya Berkane Jijini Berkane nchini Morocco.

Mabao ya Black Queens yamefungwa na mshambuliaji waTrabzonspor ya Uturuki, Princella Adubea dakika ya 12, kiungo wa Al Ahli ya Saudi Arabia, Alice Kusi kwa penalti dakika ya 63, mshambuliaji wa Fleury ya Ufaransa, Evelyn Badu dakika ya 87 na winga wa London City Lionesses ya England, Chantelle ‘Chaney’ Boye-Hlorkah dakika ya 90, wakati bao pekee la Twiga Stars limefungwa na kiungo wa JKT Queens ya nyumbani, Stumai Abdallah Athumani dakika ya 41.

Kwa matoke ohayo, Tanzania inamaliza mkiani mwa Kundi C ikiwa imevuna pointi moja tu kufuatia sare ya 1-1 na mabingwa watetezi, Afrika Kusini huku mchezo mwingine wakifungwa 1-0 na Mali.

Mchezo mwingine wa mwisho wa Kundi C leo, mabingwa watetezi, Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ wameitandika Mali ‘The Female Eagles’ mabao 4-0 Uwanja wa Honneur mjini Oujda.

Bahati nzuri timu nyingine zote za Kundi C zinafuzu Robo Fainali, Banyana Banyana kama vinara kwa pointi zao saba, Black Queens kama washindi wa pili kwa pointi zao nne na The Female Eagles kama washindi watatu Bora kwa pointi zao nne pia wakiipiku Senegal ya Kundi A na Botswana ya Kundi B zilizomaliza na pointi tatu.

Tanzania ilikuwa inashiriki Fainali za Afrika kwa mara ya pili kihistoria baada ya mwaka 2010 nchini Afrika Kusini ambako walifungwa mechi zote, 2-1 na wenyeji, Banyana Banyana, 3-2 na Mali na 3-0 na Nigeria na kutolewa hatua ya makundi pia.