MKANDARASI wa mradi wa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira jijini Arusha, China Railway Construction Engineering Group Company Limited, amesheherekea kukamilika kwa hatua ya mwisho ya kumwaga zege kwenye jengo la uwanja ikiwa ni siku 360 tu tangu mkataba ulipoanza mwaka jana.
Tukio hilo lilifanyika jana, Julai 19 kwenye viwanja hivyo jijini Arusha likiambatana na kuinuliwa rasmi kwa nguzo ya paa la chuma la kwanza, ikiwa ni hatua kubwa kuelekea ukamilishaji wa mradi huo kwa hatua ya pili ya kufunika uwanja na kufanya finishing.
Kazi ya umwagaji zege imejumuisha zaidi ya mita za ujazo 50,000 za zege ambazo zimekamilika kwa ubora na vimango ndani ya miezi 8 tangu umwagaji wa zege ulipoanza rasmi. Hatua inayofuata ni uwekaji wa paa, finishing za ndani, mifumo ya teknolojia na viti.
Tukio hilo limehudhuriwa afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya mkandarasi duniani kote Bw. Wang Yusheng na viongozi wa juu wa kampuni hiyo pamoja na viongozi wa serikali akiwemo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma.