Fountain Gate yanusurika kushuka daraja

TIMU ya Fountain Gate imejinusuru kuteremka daraja baada ya ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Stand United katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa mwisho wa kuwania nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.

Mabao ya Fountain Gate yamefungwa na Ellie Mokono dakika ya 51 na William Edgar dakika ya 90’+1 na kwa matokeo hayo, Stand United inatupwa nje kwa kichapo cha jumla cha 5-1 kufuatia kufungwa 3-1 kwenye mchezo wa kwanza Ijumaa iliyopita Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

Fountain Gate sasa inakamilisha idadi ya timu 16 za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu ujao - nyingine ni Yanga, Simba, Azam FC, Singida Black Stars, Tabora United, Coastal Union, Dodoma Jiji, JKT Tanzania, Mashujaa FC, Namungo FC, Pamba Jiji FC, KMC, Tanzania Prisons, Mbeya City na Mtibwa Sugar.

Ikumbukwe Fountain Gate waliporomoka kwenye mchujo wa Ligi Kuu baada ya kutolewa na Tanzania Prisons, wakati Stand United walifuzu mchujo wa Championship baada ya kuitoa Geita Gold.