TIMU ya Fluminense ya Brazil imefanikiwa kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Al-Hilal ya Saudi Arabia usiku wa kuamkia leo Uwanja wa Camping World, Orlando, Orange County, Florida, Marekani.
Mabao ya Fluminense yamefungwa na viungo Matheus Martinelli Lima dakika ya 40 na Hércules Pereira do Nascimento dakika ya 70, wakati bao pekee la Al Hilal limefungwa na Mbrazil pia, mshambuliaji Marcos Leonardo Santos Almeida dakika ya 51.
Wachezaji wa A Hilal hawakuwa wakifurahishwa na maamuzi mengi ya Refa Mholanzi Danny Makkelie kwenye mchezo huo, mara kadhaa akigoma kwenda kupata msaada wa marudio ya picha za video (VAR) kwenye matukio ambayo yangeinufaisha timu ya Saudi Arabia.
Fluminense sasa itakutana na mshindi wa Robo Fainali ya pili kati ya Palmeiras ya Brazil pia na Chelsea ya England zitakazomenyana baadaye Alfajir Uwanja wa Lincoln Financial Field, Philadelphia.