TIMU ya Chelsea ya Uingereza imefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Palmeiras ya Brazil Alfajir ya leo Uwanja wa Lincoln Financial Field, Philadelphia, Marekani.
Mabao ya Chelsea yamefungwa na kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa England, Cole Jermaine Palmer dakika ya 16 na kipa Mbrazil, Weverton Pereira da Silva aliyejifunga dakika ya 83.
Bao pekee la Palmeiras limefungwa na winga chipukizi wa umri wa miaka 18, Estêvão Willian Almeida de Oliveira Gonçalves anayefahamika zaidi tu kama Estêvão Willian au Estêvão ambaye ya 53.
Chipukizi huyo amefunga bao hilo akicheza mechi yake ya mwisho Palmeiras kabla ya kuhamishia makali yake Stamford Bridge, kwani taarifa zinasema uhamisho wake kwenda Chelsea umekamilika na atatangazwa rasmi muda wowote.
Chelsea sasa itakutana na wapinzani wengine kutoka Brazil, ambao ni Fluminense waliowatoa Al-Hilal ya Saudi Arabia usiku wa jana katika Robo Fainali ya kwanza ya michuano hiyo Uwanja wa Camping World, Orlando, Orange County, Florida.
Mabao ya Fluminense yalifungwa na viungo Matheus Martinelli Lima dakika ya 40 na Hércules Pereira do Nascimento dakika ya 70, wakati bao pekee la Al Hilal lilifungwa na Mbrazil pia, mshambuliaji Marcos Leonardo Santos Almeida dakika ya 51.
Wachezaji wa A Hilal hawakuwa wakifurahishwa na maamuzi mengi ya Refa Mholanzi Danny Makkelie kwenye mchezo huo, mara kadhaa akigoma kwenda kupata msaada wa marudio ya picha za video (VAR) kwenye matukio ambayo yangeinufaisha timu ya Saudi Arabia.