CECAFA waanzisha mshindani mapya, kuchezwa Karatu

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeandaa michuano ya mataifa manne, Kenya, Tanzania na Uganda pamoja na waalikwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inayotarajiwa kuanza Julai 21 hadi 27 Uwanja wa Karatu Jijini Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, Mkenya John Auka Gecheo amesema kwamba michuano hiyo ni fursa nzuri ya maandalizi kwa timu za ukanda wake, Kenya na Uganda na Tanzania kupata maandalizi ya mwisho kabla ya Fainali za Kombe la Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).

Fainali za CHAN zinatarajiwa kuanza Agosti 2 hadi 30, mwaka huu zikiwa zinaandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Kenya, Tanzania na Uganda.

Katika michuano hiyo ya mataifa manne, Tanzania itaanza na DR Juni 21 Saa 10:00 jioni, baada ya Kenya kucheza na Uganda Saa 7:00 mchana, wakati Julai 24 Uganda watacheza na DRC Saa 7:00 mchana, kabla ya Tanzania kumenyana na Kenya Saa 10:00 jioni.

Julai 27 Kenya itamenyana na DRC kuanzia Saa 7:00 mchana kabla ya Tanzania kumenyana na Uganda kuhitimisha michuano hiyo ya CECAFA.

Katika CHAN Kundi A kuna Kenya, Morocco, Angola Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia, Kundi B kuna Tanznaia, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), wakati Kundi C linazikutanisha Uganda, Niger, Guinea, Algeria na Afrika Kusini wakati Kundi D kuna Senegal, Kongo, Sudan na Nigeria.