WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba amempongeza mmiliki wa kampuni ya Azam Media Limited, Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye sekta ya michezo nchini ambao umekuwa chachu ya maendeleo ya michezo nchini.
Waziri Dk, Nchemba aliyasema hayo jana Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26 yenye jumla ya Shilingi za Tanzania Trilioni 56.49.
“Nimpongeze kipekee Mzee Said Salim Bakhresa kwa uwekezaji mkubwa katika tasniya michezo. Huyu ni wa mfano, uwekezejai wake umekuwa chachu ya maendeleo ya michezo nchini, hususan kupitia matangazo ya moja kwa moja, yaani mbashara,” amesema Dk Nchemba na kuongeza.
“Ni ukweli usiopingika kuwa Maisha ya watu hayawezi kukamilika bila kuwa na furaha, hilo tumeliona kupitia Azam TV, ambayo siyo tu imefanya kila mtu kuzungumzia mpira wa miguu, bali wanazungumzia na maisha mengine, wachezaji wa ngumi, mpira wa miguu pamoja na filamu,”
Waziri Dk Nchemba amesema kwamba japokuwa Azam Media Limited ni Kampuni Binafsi inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Bakhresa na familia yake – lakini imekuwa kama ya umma.
“Licha ya kuwa Kampuni hii ni binafsi, lakini kwa sasa imekwishakuwa kama mali ya umma kutokana na umuhimu wake katika jamii yetu na kwa kweli Mzee Bakhresa aheshimiwe,” ameongeza.