Na Prince Hoza
TIMU ya Young Africans imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa mara ya nne mfululizo na mara ya 31 jumla baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya watani, Simba SC jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Pongezi kwa kiungo kutoka Ivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua aliyefunga bao la kwanza kabla ya kuseti bao la pili lililofungwa na mshambuliaji wa KImataifa wa Tanzania, Clement Francis Mzize, yote kipindi cha pili.
Ushindi wa Yanga haukuwa na shaka hata kidogo kwani umetokana na juhudi zake ndani ya uwanja, mchezo huo ulichezeshwa na mwamuzi wa kimataifa kutoka nchini Misri Amin Mohamed Omary.
Mwamuzi huyo alisaidiwa na washika vibendera wawili wa kushoto na kulia ambao wote wanatoka wakati kamisaa ametoka Somalia
Mchezo huo ulikuwa uchezwe Juni 15 lakini uliahirishwa baada ya Yanga kususia mechi na ikabidi Rais wa nchi, Dkt Samia Suluhu Hassan awaite Ikulu mjini Dodoma kuzungumza na timu zote mbili Yanga na Simba na hatimaye kupangwa kwa tarehe nyingine.
Mchezo huo umeangukia Juni 25 na Simba itakutana na kipigo cha mabao 2-0, Yanga walishikiria msimamo wao wa kutopeleka timu Juni 15 baada ya Simba kugomea dabi ya Machi 8 ambapo wenyewe wanadai kwamba walizuiwa kuingia uwanjani na makomandoo wa Yanga.
Vuta nikuvute ya dabi itachezwa lini ikaamuliwa na timu hizo mbili zilitakiwa kushuka uwanjani Juni 25 kukamilisha mechi zao za 30 za Ligi Kuu bara ambapo pia alijulikana bingwa wa msimu huu.
Kabla ya kukutana wao kwa wao, Yanga wametoka kupata ushindi mara mbili na zote ikishinda mabao 5-0, Yanga waliwafunga Tanzania Prisons katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kabla ya kuifunga Dodoma Jiji uwanja wa New Amaan Stadium Zanzibar.
Lakini watani zao Simba nao wamepata ushindi mechi mbili mfululizo ila ni tofauti na wenzake Yanga, Simba iliifunga KenGold mabao 5-0 na baadaye ikaifunga Kagera Sugar bao 1-0.
Mechi zote zilifanyika uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, kuelekea dabi, Yanga walijichimbia Zanzibar wakati Simba walikaa jijini Dar es Salaam, juzi Yanga walifanya mazoezi yao uwanja wa Mkapa wakati Simba walifanya mazoezi uwanja wao wa MO Simba Arena, uliopo Bunju.
Wengi hawakuamini kama mechi hiyo itafanyika, kwani Simba walisusa kwenda kwenye mkutano na waandishi wa habari juzi, kitendo cha Simba kususia press, kuliwafanya watu wengi kupata hofu ya timu kutoingia uwanjani.
Lakini jana mchezo umefanyika na Simba ikapokea kichapo cha mabao 2-0 na kila aliyeshuhudia mchezo hakuna hata mmoja anayeweza kusema kwamba Yanga walibebwa au Simba walionewa.
Katika mchezo huo Simba walianza vema kwa kulisakama lango la Yanga lakini kwa umakini mkubwa wa safu ya ulinzi ya Yanga uliondoa mashambulizi yote, hadi mapumziko timu zote zilikuwa nguvu sawa.
Kipindi cha pili Yanga waliongeza kasi na kufanikiwa kupata mabao yote mawili, moja likiwa la penalti ya halali kabisa na lingine likifungwa kwa juhudi za Pacome Zouzoua ambaye jana alikuwa nyota wa mchezo.
Nisisikie malalamiko yoyote kwa Wanasimba, ya kumlaumu mwamuzi kwani alichezesha vizuri, wala wanachama au mashabiki wa Simba kumshutumu kiongozi wa timu hiyo kwamba amehujumu timu.
Tumezoea kusikia lawama kwa wanachama au mashabiki kwa viongozi na hasa anayelalamikiwa sana Murtaza Mangungu ambaye ni mwenyekiti wa klabu hiyo, sitaki kusikia lawama kwani mpira umechezwa hadharani na Simba kufungwa kihalali..
ALAMSIKI