Rufaa ya Guinea yatupiliwa mbali CAF

KAMATI ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeitupilia mbali Rufaa ya Shirikisho la Soka Guinea (GFF) dhidi ya Tanzania juu ya mchezo wa mwisho wa Kundi H kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu nchini Morocco.

Tanzania iliifunga Guinea 1-0 Novemba 19, mwaka 2024 bao la mshambuliaji wa Al Talaba ya Iraq, Simon Happygod Msuva dakika ya 61 akimalizia pasi nzuri ya kiungo wa Yanga ya nyumbani, Dar es Salaam, Mudathir Yahya Abbas. Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo, Guinea iliyoongozwa na mshambuliaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, Serhou Yadaly Guirassy ilimkatia rufaa beki Ibrahim Mohamed Ame kwamba hakuwa raia wa Tanzania.

Hata hivyo, baada ya kuthibitishiwa uraia wake kufuatia malalamiko yao ya awali Kamati ya Nidhamu ya CAF — wakabadilisha madai yao na kukata Rufaa Kamati ya Rufaa ya Bodi hiyo ya soka Afrika wakisema alivaa jezi tofauti na iliyoandikwa kwenye orodha ya wachezaji, hivyo iliwavuruga na kusababisha wapoteze mechi hiyo.