ANGOLA MABINGWA COSAFA

TIMU ya taifa ya Angola imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji, Afrika Kusini jioni ya leo Uwanja wa Toyota, Free State Jijini Bloemfontein.

Shujaa wa Palancas Negras kwa mara nyingine leo ni mshambuliaji Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depú’ anayechezea klabu ya Vojvodina ya Ligi Kuu ya Serbia kutoka Gil Vicente ya Ureno aliyefunga mabao mawili dakika ya 43 na 62.

Bao la tatu la Angola pia limefungwa na nyota anayecheza Ligi Kuu ya Serbia, winga Felício Mendes João Milson Red Star Belgrade dakika ya 81 – na hilo linakuwa taji la pili mfululizo kwa Swala Weusi Wakubwa na la tano mfululizo jumla baada ya awali kutwaa miaka ya 1999, 2001, 2004 na 2024.

Depu mwenye umri wa miaka 25 anamaliza michuano ya mwaka huu akiwa amefunga nane na kuwa Mfungaji Bora akifuatiwa kwa mbali na Mzimbabwe, Thandolwenkosi Ngwenya, Mcomoro Ibrahim Madi na Andy Magagula wa Eswatini waliofunga mabao mawili kila mmoja