Simba na Stellenbosch kupigwa New Amaan Stadium, Zanzibar

Kikosi cha Simba kitautumia uwanja wa New Amaan Complex uliopo visiwani Zanzibar kwenye mchezo wake wa nyumbani wa nusu fainali ya Kombe la shirikisho Afrika (CAFCC) dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, mchezo utakaopigwa Jumapili ya April 20.

Klabu ya Simba ilipewa saa 48 na shirikisho la Afrika CAF kuchagua uwanja mwingine wa kuchezea nusu fainali yake dhidi ya Stellenbosch FC tofauti na uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya uwanja huo kuharibiwa na mvua iliyonyesha kwenye mchezo wa robo fainali ya pili dhidi ya Al Masry, Kwa maana hiyo uwanja wa Benjamin Mkapa umefungiwa na CAF licha ya kuwa serikali nao wameufungia kwa muda kwa ajili ya ukarabati hasa eneo la kuchezea (Pitch).

Kwa mujibu wa taarifa nilizonazo wakati Simba SC ikicheza nusu fainali ya kwanza visiwani Zanzibar wakati huohuo mkakati wa Serikali kwa maana ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni kufanya jitihada za kuufanyia maboresho uwanja ili kama ikitokea Simba SC imetinga hatua ya fainali mchezo wake wa fainali upigwe Benjamin Mkapa tofauti na uwanja mwingine.

Kama Simba SC itatinga fainali ya Kombe la shirikisho Afrika (CAFCC) mchezo wa fainali ya kwanza itapigwa Mei 17 wakati fainali ya pili ya kukabidhi kombe itapigwa Mei 24.