Iwe isiwe Simba itatinga nusu fainali - Azim Dewji

Mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji amewataka mashabiki wa timu hiyo kuamini kuwa itapata matokeo mazuri katika mechi ya marudiano dhidi ya Al Masry ya Misri, Aprili 9, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam ambayo yataipeleka hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika licha ya kufungwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ugenini.

Matokeo ya mchezo uliopita uliofanyika katika Uwanja wa Suez, Misri yanailazimisha Simba kuhakikisha inapata ushindi wa angalau mabao 3-0 ili isonge mbele na kutinga nusu fainali.

“Hakuna kitu kitamu kama kupata kitu wakati ukiwa hauna matumaini. Ukiwa na matumaini furaha inakuwa kiasi kwa hiyo tunawaomba wajitokeze kwa wingi ili tuweze kuwapa furaha.

"Tulicheza mpira mzuri kwa bahati mbaya hatukuwa na bahati lakini kwa nyumbani hapa Mungu akijalia tutacheza vizuri na tutarudisha magoli.,"

"Kwanza timu zote za bara la Afrika zinauogopa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwamba hatoki mtu salama kwa hiyo wanakuja na hofu hiyo na pili hiyo timu waliona tulivyocheza. Uwanja wa Mkapa ni mkubwa kidogo kuliko uwanja wao hivyo hapa kutanuka inakuwan ni vizuri zaidi.’ amesema Dewji