Na Prince Hoza
KWANZA nianze kwa kuwapa pongezi Singida Black Stars ina maana hongera hizi nazipeleka kwa viongozi wa klabu hiyo na wapenzi na mashabiki kwa uvumilivu wao mkubwa na kuweza kukamilisha uwanja wao.
Hapa nchini ni vilabu vichache ambavyo vinamiliki uwanja wao aidha uwe wa kufanyia mazoezi ama mechi za mashindano kwa mfano Klabu ya Azam FC inayomiliki uwanja wake wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Singida Black Stars ya mkoani Singida ni miongoni mwa vilabu hapa nchini inayoshiriki Ligi Kuu bara ambayo inamiliki uwanja wake, ni jambo la kuwapongeza kwani kuna vilabu vingine havina uwanja wake.
Simba na Yanga ndio klabu kubwa hapa nchini na ambavyo vimejizolea mashabiki wengi lakini mpaka sasa havina uwanja wake ambao vinaweza kujivunia navyo, licha kwamba Yanga SC yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani Kariakoo jijini Dar es Salaam inalalama haina uwanja wake wa mazoezi na mechi za mashindano.
Simba SC pia ya Kariakoo mtaa wa Msimbazi na Agrey jijini Dar es Salaam haina uwanja wake binafsi wa kuchezea mazoezi na mechi za mashindano, Simba kidogo wanaweza kujivunia uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju A jijini Dar es Salaam, lakini Bado hawana uwanja pasee.
Kwa kifupi Simba na Yanga zote zina umri ya miaka 90 sasa hawana uwanja, lakini timu changa kama za Azam FC na Singida Black Stars zinamiliki uwanja wake.
Uwanja wa Azam Complex ndio ambao naweza kusema kwamba ni uwanja kwa maana umekamilika, uwanja wa Azam Complex unatumika kwa kuchezea mazoezi na mechi za mashindano kuanzia ya ligi za nyumbani na kimataifa.
Uwanja huo umepitishwa na Shirikisho la soka barani Afrika, CAF, uwanja ni bora na ukitaja viwanja vizuri Afrika mashariki nao upo miongoni mwao, KMC Complex unamilikiwa na Manispaa ya Kinondoni wakati uwanja wa Meja Isamuyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam unamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa, JKT.
hakuna timu nyingine inayomiliki uwanja wake ukiziondoa Azam na Singida, katika makala yangu ya leo nachukua nafasi kuwapongeza Singida Black Stars kwa kukamilisha uwanja na kufanya uzinduzi Machi 24.
Klabu hiyo ilifanya uzinduzi wake na kucheza mechi ya kirafiki na Yanga SC ya jijini Dar es Salaam, ningefurahi sana kuona uzinduzi wake wa uwanja wangecheza na Azam FC ambao nao wanamiliki uwanja.
Zamani Yanga walikuwa na uwanja wao wa mazoezi na mechi za kirafiki uitwao Kaunda Stadium uliopo pale pale kwenye jengo lao mitaa ya Twiga na Jangwani, lakini miundombinu haikuwa mizuri ukaondoka na maji (mafuriko).
Wakati nikiwapa pongezi Singida Black Stars kwa kufanikisha uzinduzi wa uwanja, nasikitika kwamba Singida Black Stars walifanya haraka kufanya uzinduzi wakati walitakiwa kusubiri Ili kukamilisha wote.
Uwanja huo waliouzindua hauna uwezo wa kutumika kwani kwa mujibu wa Bodi ya Ligi utakuwa umekosa sifa, Ili uwanja uweze kutumika kwenye michezo ya Ligi Kuu bara lazima uwe na majukwaa.
Uwanja wa Airtel Stadium hauna majukwaa hivyo hauna faida kwa timu hiyo, faida ya Singida Black Stars kuwa na uwanja ni kufanyia mazoezi tu, tunataka timu zinazomiliki uwanja wake ambao utatumika kwenye mazoezi na mechi za mashindano.
Sio vilabu peke yake tunavitaka kujenga uwanja wake binafsi hata vyama vya soka vya mikoa au TFF hata Bodi ya Ligi kumiliki uwanja wake binafsi, niwatoe wasiwasi kwamba walichofanya Singida Black Stars ni kitu kizuri na linafaa kuigwa, ila ni vizuri zaidi kama uwanja ukikamilika wote na majukwaa ni vizuri zaidi.
ALAMSIKI