LIGI YA MCHEZO WA DRAFT KUANZISHWA TABATA

Na Ikram Khamees. Dar es Salaam

Klabu ya michezo ya Mtambani SC imetangaza kuanzisha michuano ya kumpata bingwa wa mchezo wa bao (Draft) kwa maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na mtandao huu, Mratibu wa shindano hilo Musa Benjamin amesema jumla ya watu 14 watashiriki shindano hilo litakalojulikana kama 'Ligi ndogo' ambapo bingwa atajinyakulia zawadi nono pamoja na kikombe chenye thamani ya shilingi 50,000.

Benjamin amedai nia na madhumuni ya kuanzisha mashindano hayo ni kuleta burudani kwa wakazi wa Tabata na pia kuendeleza mchezo huo ambao umesahailika, ameongeza kuwa watu wengi wanaelekeza nguvu zao kwenye mpira wa miguu na kusahau michezo mingine.

"Nia yetu ni kuona mchezo wa bao (Draft) unapata msisimko wake sio kila kukicha soka tu", alisema Musa Benjamin ambaye ndiye mratibu wa shindano linalotarajiwa kuanza Juni 16 au 17 mwaka huu

(Pichani) wachezaji wa bao (Draft) wakishindana, hao nao ni miongoni mwa washiriki wa ligi ndogo, (Picha na Gaudence Magwaja)