KIUNGO Muivory Coast, Peodoh Pacôme Zouzoua amesaini mkataba mpya wa kuendelea na kazi katika klabu ya Yanga hadi mwaka 2027.
Kupitia vyanzo vyake katika mitandao ya kijamii – Yanga imesema kwamba Pacome ameongeza mkataba, ambayo inazima tetesi za mchezaji huyo kuondoka.
Pacome amekuwa na wakati mzuri tangu amewasili Yanga SC Julai19 mwaka 2023 akitokea ASEC Mimosas ya kwao, Abidjan akiiwezesha timu hiyo kushinda mataji yote ya nyumbani na kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mfululizo kwa mara ka kwanza katika historia yake 2023-2024 na 2024-2025.
Kisoka Pacome aliibukia Williamsville ya kwao mwaka 2016, kabla ya kujiunga na Sparta Prague B ya Jamhuri ya Czech mwaka 2017 ambako alicheza kwa misimu miwili na kurehjea nyumbani kujiunga na SC Gagnoa mwaka 2019.
Hata kabla ya msimu kuanza, ndani ya wiki moja ya kujiunga na SC Gagnoa akachbukuliwa na Daugavpils ya Latvia ambako alicheza hadi mwaka 2020 akarejea Ivory Coast kujiunga na Africa Sports hadi mwaka 2021 akahamia ASEC.