TIMU ya Chelsea ya England imefanikiwa kuingia Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fluminense ya Brazil usiku wa Jumanne Uwanja wa MetLif, East Rutherford, Bergen County, New Jersey, Marekani.
Mabao ya The Blues yaliyoizamisha Time de Guerreiros (Timu ya Mashujaa) yamefungwa na mchezaji wao wenyewe wa zamani, mshambuliaji Mbrazil João Pedro Junqueira de Jesus maarufu tu kama João Pedro (23) dakika ya 18 na 56.
Sasa Chelsea ambayo inafundishwa na Kocha Mtaliano, Enzo Maresca (45) itakutana na mshindi wa Nusu Fainali ya pili kesho kati ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa na Real Madrid ya Hispania hapo hapo Uwanja wa MetLife.
Fainali itapigwa Julai 13 hapo hapo Uwanja wa MetLife.
João Pedro ni mchezaji aliyeanzia soka katika timu ya vijana ya Fluminense mwaka 2011 hadi 2019 alipopandishwa timu ya wakubwa, kabla ya kuuzwa Watford ya England mwaka 2020.
Watford nayo ilimuuza João Pedro Brighton & Hove Albion mwaka 2023 ambayo ndiyo iliyowauzia Chelsea huyo Julai 2 tu mwaka huu, 2025.