Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz KI, ameingia kwenye kinyang'anyiro cha tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka katika African Golden Awards, akichuana na nyota wakubwa wa Afrika akiwemo Mohamed Salah wa Liverpool na Sadio Mane wa Al Nassr.
Hii ni mara ya pili kwa KI kuwaniwa kwenye tuzo hizo, baada ya awali kujumuishwa kwenye kipengele cha ‘kapo’ bora ya mwaka pamoja na mkewe, Hamisa Mobetto. Tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Aprili 5 nchini Kenya.
Nyota huyo wa Burkina Faso ni miongoni mwa wachezaji 16 walioteuliwa kwenye kipengele hicho, akichuana na mastaa kama Riyad Mahrez (Al-Ahli), Ademola Lookman (Atalanta), Kalidou Koulibaly (Al-Hilal), Amad Diallo (Man United), Achraf Hakimi (PSG), Thomas Partey (Arsenal) na Andre Onana (Man United). Wengine ni Franck Kessie (Al-Ahli), Michael Olunga (Al-Duhail), Ronwen Williams (Mamelodi Sundowns) na Mohamed Kudus (West Ham United).
Aziz KI ameendelea kuwa mhimili wa Yanga tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast msimu wa 2022/23. Katika msimu wake wa kwanza, alifunga mabao tisa kwenye mechi nane, kabla ya kutwaa kiatu cha dhahabu msimu uliofuata kwa mabao 21. Msimu huu, tayari amefunga mabao saba.