MHESHIMIWA TEMBA, CHEGGE KUREJEA UPYA

WAKALI wa muziki wa kizazi kipya nchini kutoka kundi la TMK Wanaume Family, Said Juma ‘Chege’ na Amani Temba ‘Mheshimiwa Temba’ wanatarajia kuachia kibao kipya cha ‘Tufurahie’.

Wakali hao wamekuwa wakitamba na vibao mbalimbali vikiwemo ‘Tutaonekanaje’ na ‘Kichwa Kinauma’ ambavyo vinatamba zaidi katika vituo mbalimbali vya luninga na redio nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kiongozi wa kundi hilo, Said Fella alisema ngoma hiyo wanatarajia kuisambaza hivi karibuni katika vituo mbalimbali vya redio kabla hawajaipeleka videoni.

“Mkubwa na wanawe tuko kazini muda wote na tunaahidi kuendelea kutoa burudani kwa wapenzi na mashabiki wetu kwani huu bado ni mwanzo tu,” alisema Fella.

Fella alisema kuwa wanawaomba mashabiki wao waupokee wimbo huo kwa mikono miwili kutokana na uandaaji wake ambao alisema ni wa hali ya juu, ukiwa umeimbwa kwa ushirikiano na msanii mwingine wa kundi hilo, YP.

Fella alisema wimbo huo umerekodiwa katika studio ya Tudy na kwamba wataupeleka videoni haraka iwezekanavyo ili kuwapa raha zaidi wapenzi na mashabiki wao.