
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Alisema baada ya kampuni hizo kuwadhulumu wasanii kwa muda mrefu, zimeanza kuwalipa fedha angalau hivi sasa kufuatia wao wabunge kupigia keleleni wizi huo unaowaumiza wasanii na kuwanufaisha wenye makampuni hayo.
Zitto alimtolea mfano msanii wa kizazi kipya, Hamis Mwinjuma a.k.a MwanaFA kwamba wiki hii amepewa Sh. milioni 18 kama mapato yake ya miezi mitatu kutokana na mauzo ya miito ya simu, jambo ambalo zamani halikuwa likifanyika. "Hii inathibitisha namna walivyokuwa wakidhulumiwa kwa muda mrefu, wameanza kuwalipa sasa baada ya sisi kupiga kelele," alisema.
Zitto alisema kwamba kampuni zinazouza miito hiyo ya simu hazitoi taarifa za mauzo kwa wasanii na wanatumia uelewa mdogo wa wasanii kuwasainisha mikataba inayowanyonya.
Alisema matokeo yake ni kwamba msanii hupata kiasi cha asilimia mbili tu (2.5%) ya mapato ghafi ya kazi yake wakati biashara hiyo ina thamani ya takribani Sh bilioni 44 kwa mwaka.
NIPASHE ilipoongea na MwanaFA alisema kwamba alishangazwa na kulipwa kiasi hicho hivi sasa kwani kabla ya wabunge kuwapigania alikuwa akilipwa kati ya Sh.300,000 na Sh.400,000.
"Tumeibiwa sana na inaumiza kwa kweli. Tunatoka jasho lakini wananufaika watu wengine, harakati hizi zinaweza kutusaidia tukanufaika kulingana na jasho letu," alisema rapa huyo.
Naye Sharon Sauwa, anaripoti kutoka dodoma kuwa serikali imekiagiza Chama cha Hakimiliki Nchini (Cosota), kukaa na kuangalia jinsi wasanii wa muziki watakavyonufaika na miito ya simu (Ring Tones) inayotumiwa na wateja kwenye mitandao ya simu nchini.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2013/2014, bungeni mjini Dodoma jana.
Bila kufafanua, Dk Kigoda alisema nchi nyingine wamekuwa wakitoza hadi ya asilimia 10 ya mapato yanayotokana na miito ya simu kwa ajili ya kuwalipa wasanii wanaomiliki muziki huo.
Kwa upande wa Msemaji wa kambi ya Upinzani kuhusiana na Wizara hiyo, Highness Kiwia, alisema wasanii wengi nchini na hasa wasanii vijana wa muziki wananyonywa na makampuni makubwa yenye nguvu kwa sababu Cosota haina dhamira kutetea na kulinda haki za wasanii.
“Kambi ya upinzani Bungeni inapendekeza kuwa Cosota itoe kanuni kudhibiti biashara ya nyimbo za wasanii kama miito. Nchini Marekani miito ya simu ni kazi za kisanaa na wasanii hulipwa si chini ya asilimia 10 ya mapato kutoka kwenye mitandao ya simu,”alisema.
Alisema hapa nchini hakuna kanuni za kuongoza biashara hii ambayo imetokana na maendeleo ya teknolojia.
“Tunataka uwazi na haki katika biashara hii na Ringtones na ijulikane kiasi gani cha kodi kinapatikana,” alisema.
Aidha, Dk. Kigoda alisema Cosota imekusanya mirahaba ya jumla ya Sh. milioni 98.8 .
“Kati ya hizo, Sh. milioni 88.0 ziligawiwa mwezi Machi mwaka 2013 zikiwa ni makusanyo ya Julai-Desemba mwaka 2012 na zilizobaki zitaingia katika mgao wa Julai mwaka 2013,” alisema.
Pia alisema hadi kufikia Januari mwaka huu, Cosota imepokea na kusikiliza kesi na kusimamia mashitaka yanayohusiana na ulipaji wa mirahaba.
“Jumla ya mashtaka yaliyopokewa ni 26 dhidi ya kazi za hakimiliki na kushughulikia migogoro 23 ya wasanii mbalimbali na migogoro 14 imepatiwa ufumbuzi,” alisema.