Na Prince Hoza
MWENYEKITI wa Bodi ya Simba SC, Mohamed Gulam Dewji amesema kwamba ndani ya miaka saba ya uwekezaji wake ametumia zaidi ya Sh. Bilioni 87.
Mo Dewji ameposti video usiku akizungumzia mchango wake katika klabu hiyo kuanzia mwaka 2017 hadi 2024 akitoa mchanganuo wa fedha alizotoa ndani ya kipindi hicho.
“Kutoka mwaka 2018 hadi leo nimewekeza Shilingi Bilioni 45 kwa ajili ya mishahara, usajili, maandalizi ya timu na mahitaji mengine ya uendeshaji,”.
“Pia nimechangia Shilingi Bilioni 20 kama sehemu ya ununuzi wa hisa asilimia 49 ndani ya Simba Sports Club. Na mara nyingine nimekuwa nikitoa msaada nje ya mfumo rasmi kila palipojitokeaa uhitaji wa dharula,”.
“Kuanzia mwaka 2017 hadi 2024 nimetumia takriban Bilioni 22 katika misaada ya dharula na hivyo kufanya jumla ya mchango wangu wa Simba kufikia Shilingi Bilioni 87,”.
“Hivyo kusema Mo hatoi hela ni kauli ya kupotosha yenye mwelekeo wa chuki. Tuachane na fitina zisizo na msingi, tujenge palipotoboka, tuzibe ufa panapovuja na tusonge mbele bila kuonyeshana vidole,”.
“Simba ni yetu sote na mafanikio yake yanategemea mshikamano wetu. Simba bado ipo katika hatua ya ujenzi, pamoja na changamoto zote tumefanikiwa kufika Fainali, hatua muhimu kwa timu inayozidi kulia na kuimarika,”amesema.
Dewji amesema kwamba kuelekea msimu ujao watajenga timu imara kwa usajili makini wa wachezaji bora kuiongezea nguvu timu ili irejeshe makali yake.
Amesistiza dhamira yake ya kuiwezesha Simba kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na kuifanya siku moja iwe klabu namba moja baraka Afrika.
Ni kweli- kauli yake nimeielewa na anastahili pongezi kwa kile alichowanyia Wanasimba, kuanzia mwaka 2017 mpaka sasa Simba imekuwa timu ya mafanikio ndani na nje.
Uwepo wa MO umekuwa na faida sana ndani ya klabu hiyo kwani mbali ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bara mara nne mfululizo, lakini tumeshuhudia timu hiyo ikifika robo fainali ya Ligi ya mabingwa mara tano na kufika fainali ya kombe la Shirikisho Afrika.
Tumeshuhudia Simba ikisajili wachezaji mashuhuri ambao walikonga nyoyo za mashabiki wake na Tanzania kwa ujumla, hata mahasimu wao Yanga walivutiwa na wachezaji wa Simba ambao MO alihusika kuwaleta kupitia fedha zake.
Nyota ambao walikuwa gumzo ni pamoja na Clatous Chama ambapo Yanga wakaamua kumchukua, mwingine Luis Miquissone ambaye alichukuliwa na timu ya Al Ahly ya Misri.
Ingawa zipo dosari ambazo MO anaweza kushutumiwa nazo hasa kushindwa kusimamia vema fedha anazopeleka kwani zimesababisha Simba kushindwa kufikiwa malengo yake ipasavyo.
Kufungwa mara tano mfululizo na mtani wake Yanga kimewaumiza sana mashabiki wa Simba, hakuna kipindi kibaya ambacho Simba wamewahi kupitia kama hiki cha utawala wa MO.
Kwa sasa hivi Yanga imekuwa mbabe kwa Simba na imefikia hatua wanaomba hadi mechi ya kirafiki, jambo ambalo halijawahi kutokea, dhama za MO, Simba inazidiwa na Yanga kwenye usajili wakati tajiri wake akitajwa nambari moja hapa nchini, na pia akidai amemwaga hela zinazofikia bilioni 87.
ALAMSIKI