Mwamuzi wa kati, Amina Kyando kutoka Morogoro na mwamuzi msaidizi namba mbili (2), Abdalah Bakenga kutoka Kigoma wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira kwenye mchezo wa Ligi Kuu kati ya Pamba Jiji Fc dhidi ya Singida Black Stars.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi, pamoja na matukio mengine, waamuzi hao walishindwa kutafsiri sheria katika tukio la kipa wa klabu ya Singida Black Stars kudaka mpira akiwa nje ya eneo la penati, hivyo kutotoa adhabu yoyote kwa kipa huyo.
Waamuzi hao pia walionekana kutetereka na kutojiamini hata katika kufanya maamuzi yaliyo sahihi katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 1-1 katika dimba la CCM Kirumba, Mwanza.
